Video:Ziara ya Dar Mpya yamkalia pabaya RC Makonda....Atuhumiwa Kuwadhalilisha Watumishi wa Umma kwa Kuwaita Vichaa

KAULI mbalimbali zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa ziara zake zimezua taharuki jijini humo.
Kwa nyakati mbalimbali wakati wa ziara zake, Makonda anadaiwa kutoa kauli za vitisho hasa kwa watumishi wa umma.
Kutokana
na hali hiyo, Chama cha ACT-Wazalendo kimemshtaki mkuu huyo wa mkoa
katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Utawala Bora ili
imuwajibishe.
Katika
taarifa yake iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam
na Katibu wa Ngome ya Wanawake wa chama hicho, Esther Kyamba alisema
kauli alizozitoa Makonda zimewadhalilisha watumishi hao.
“Tumesikitishwa
na kuhuzunishwa na kauli zisizo za kiuongozi na zisizozingatia kanuni
za maadili ya utumishi wa umma zinazoendelea kutolewa na RC Makonda.
“Jana
(juzi), katika mkutano anaouita wa kutatua kero kwa wakazi wa Dar es
Salaam aliendelea kushindwa kutatua kero na badala yake kuongeza kero ya
kudhihaki, kudhalilisha kukejeli na kutukana hadharani wananchi
anaowaongoza na watumishi anaowasimamia kitendo ambacho ni kinyume na
maadili ya Watanzania,” alisema.
Kyamba
alisema kitendo cha Makonda kumtolea lugha ya udhalilishaji Ofisa Ardhi
wa Manispaa ya Kinondoni, Rehema Mwinuka akiwa Mabwepande kwa kumtamkia
kwamba “Hawa ndio vichaa tunaohangaika nao, toka hapa”. Hakikubaliki.
“Kauli
hiyo imetushtua sana,tunalaani kwa nguvu zetu zote, kauli kama hii si
tu haikupaswa kutolewa na kiongozi mkubwa katika ngazi ya mkoa lakini
pia ni kauli mbaya ambayo ililenga kumdhalilisha Rehema na kumvunjia
heshima yake mbele ya umma,” alisisitiza.
Alisema
kutokana na udhalilishaji huo uliofanywa na Makonda, wameshawasilisha
mashtaka yao dhidi yake mbele ya Tume, wakiitaka imwajibishe kwa kitendo
chake hicho cha utovu wa nidhamu na maadili ya utumishi wa umma.
“Ngome
inamtaka mkuu huyo wa mkoa kutambua kuwa kwa kuzingatia Sheria ya
Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Maadili ya Utumishi
wa Umma, kanuni ya 65(1) inamtaka mtumishi wa umma, “kuepuka kufanya
vitendo viovu au kutamka maneno yanayolenga kuwaaibisha watumishi wa
ngazi moja, za chini yao au wa vyeo vya juu,” alisema.
Alisema
kitendo alichofanya, kumwaibisha na kumtolea lugha ya udhalilishaji,
Mwinuka ni kinyume cha Sheria na Kanuni za Utendaji katika Utumishi wa
Umma.
“Tunaitaka
Tume ifanye uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya matamshi mbalimbali
yaliyotolewa na Makonda ambayo yalikiuka sheria ya Maadili ya Utendaji
katika Utumishi wa Umma.
“Tunayataka
mashirika na asasi mbalimbali zinazosimamia haki za binadamu, haki za
jinsia na utawala bora kupaza sauti dhidi ya kauli isiyo ya kiuongozi
ya Makonda, Ngome na Chama kwa ujumla tutaendelea kuwasemea wanyonge
wote popote walipo kwa kadri ya uwezo wetu,” alisema.


