Rais Lungu wa Zambia Akataa Biashara ya Uswahiba.....Ataka Ufanisi Zaidi Bandari ya Dar es Salaam

Rais
wa Zambia, Edgar Lungu amewataka watendaji wa nchi yake na Tanzania,
kuweka siasa pembeni na kujikita kwenye biashara zitakazoinua uchumi wa
nchi hizo mbili.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku
tatu, Rais Lungu aliyetembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na
Shirika la Kusafirisha na Kupokea Mizigo la Zambia (Zamcargo), alisema
licha ya kuenzi mchango wa waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius
Nyerere na Kenneth Kaunda, watajikita zaidi kwenye biashara.
“Changamoto
mliyonayo ni kwenu uongozi na Bodi ya TPA kwa watu wa Kusini au
Mashariki au hata nje ya Afrika. Watu wa Zambia wanasema muda wa siasa
umekwisha, sasa ni muda wa maendeleo. Hatutawaunga mkono kwa sababu niko
karibu sana na Rais (John) Magufuli. Ni kweli niko karibu na Rais
Magufuli kama mlikuwa hamjui, lakini hatuwaungi mkono kwa sababu hiyo,
bali kwa ufanisi wenu,” alisema Rais Lungu.
Akizungumzia miradi ya reli ya Tazara na bomba la mafuta la Tazama, Rais Lungu alisema nayo inapaswa kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ni
kweli sisi ni ndugu lakini hatuangalii hilo. Wazambia wanataka mbolea
ifike haraka, shaba isafirishwe haraka kwenda sokoni,” alisema.
Akiwa
katika ofisi za Zamcargo, Rais Lungu alirudia wito wake wa ufanisi wa
biashara akisema hatasita kuwawajibisha watendaji wa taasisi hiyo.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema Zambia imekuwa mteja
namba moja katika usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es
Salaam.
Kakoko
alisema mwaka 2014, Zambia ilichangia asilimia 36 ya mizigo ambayo ni
sawa na tani milioni 5.2 ikiwa ni mbali ya nchi nane zinazotumia bandari
hiyo.
“Takwimu
za TPA zinaonyesha kuwa mizigo ya Zambia inayopitia hapa imekuwa
ikiendelea kila mwaka. Mwaka 2011, bandari ilipokea tani milioni 1.6 za
mizigo inayotoka na kuingia. Lakini mwaka 2014 Zambia ilipokea tani
milioni 1.9 za mizigo ya Zambia,” alisema Kakoko.
Alisema kutokana na umuhimu huo, uongozi wa TPA umekuwa ukiboresha huduma ili kufanya kazi kwa ufanisi.
“Kwa
mfano, muda wa kutoa mizigo bandarini umepunguzwa hadi siku kumi na
moja mwisho wa Oktoba kulinganisha na siku 32 zilizokuwa mwaka 2008.
Bandari pia imeboresha mfumo wa malipo ya mizigo kwa wateja wake kwa
kutumia mfumo wa kielektroniki,” alisema Kakoko.
Katika
ziara hiyo ya bandarini, Lungu aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Balozi, Augustine Mahiga, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani na katibu mkuu
wa wizara hiyo, Dk Leonard Chamuriho.
Mara
baada ya ziara hiyo Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine wa
Serikali kumsindikiza mgeni wake huyo uwanja wa ndege na kurejea Zambia.
Viongozi
wengine waliofika uwanjani hapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine. Rais Lungu aliondoka
uwanjani hapo saa 7: 40 mchana.


