KENYA: MAHAKAMA YAFUTILIA MBALI MGOMO WA MARUBANI WA KQ
MGOMO wa marubani wa shirika la ndege nchini Kenya Airways (KQ)
umefutiliwa mbali Ijumaa na mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi
(ELRC).
Ndege ya Kenya Airways aina ya Dreamliner B787 ikitua JKIA Aprili 5, 2014.
Jaji Mathew Nduma Nderi wa ELRC aliambiwa mgomo huu utailetea nchi hasara kubwa zaidi.
“Naomba mahakama isitishe mgomo huu unaotishia nchi hii kupata hasara
kubwa kwa vile KQ imeweka kandarasi na kampuni nyingi kote ulimwenguni,”
akasema wakili Geoffrey Obura anayewakilisha shirika hili la ndege
ambalo ni kauli mbiu yake ya kiutendakazi ni 'fahari ya Afrika'.
Marubani hawa walikuwa wamepanga kuanza mgomo wiki ijayo endapo wakuu wa shirika hilo la ndege 'hawatatimuliwa kazini'.
Marubani hawa kupitia kwa chama chao cha Kenya Airline Pilots
Association (Kalpa) wamekuwa wakisukuma kufutwa kazi kwa Mkurugenzi mkuu
Bw Mbuvi Ngunze pamoja na mwenyekiti wa shirika hili la ndege
linalokumbwa na uhaba wa fedha Balozi Dennis Awori.
Jaji Nduma Nderi alikubalia ombi la KQ lililoomba mgomo huo usitishwe kwa vile utaathiri huduma na safari za ndege.
Wakili Geoffrey Obura anayetetea KQ alisema hatua ya marubani hawa inalenga kulemaza kabisa safari za ndege.


