MAAJABU: JAMAA AFUNGA NDOA NA SIMU YAKE YA "SMARTPHONE" KANISANI.
Dunia ina mambo, na ukiyashangaa haya jiandae kuyastaajabu yajayo..!
Mwanaume mmoja aliyejitambusha kwa jina la Aaron Chervenak mwenye umri
wa miaka 34 na mkazi wa Los Angeles nchini Marekani, amefanya tukio la
aina yake baada ya kufunga ndoa kanisani na simu yake ya kupapasa
(smartphone).
Mwanaume huyo alisafiri hadi Vegas kulisaka kanisa moja ambalo
lilimkubalia kufunga ndoa na simu yake na kula kiapo kama ambavyo
alipaswa kula kiapo kwa mrembo aliyeyagusa maisha yake na kuamua
kumfanya mkewe wa maisha.
Akizungumzia sababu zilizopelekea yeye kufanya tukio hilo, kupitia
makala maalum ya ndoa yake hiyo, Aaron alisema kuwa ameamua kufanya
hivyo kwa sababu ya ukweli kwamba simu zimekuwa zikichukua nafasi kubwa
ya mapenzi na uhusiano na zikifanya jukumu kubwa la kuwatuliza watu
katika dunia hii.
“Kama tutakuwa wakweli, tunaunganishwa na simu katika viwango vingi vya
hisia. Tunaikimbilia kututuliza, kutulaza usingizi, kuweka unafuu kwenye
mawazo yetu. Na kwangu, huo ndio uhusiano nilionao na simu yangu hii,”
alisema Aaron.
“Kwa mantiki hiyo, simu yangu hii imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na
mimi na ndio maana nimeamua kufunga nayo ndoa,” aliongeza.
Kuhusu jinsi alivyokubaliwa kufanya tukio hilo kanisani, alisema kuwa
alijaribu kuwasiliana na uongozi wa kanisa hilo kuona kama angeruhusiwa
lakini alihakikishiwa kuwa anakaribishwa kwa mikono miwili.