Tundu Lissu,Mwigulu Nchemba Na Zitto Kabwe waguswa na msiba Arusha
Baadhi ya wanasiasa nchini wametuma salamu za rambirambi kwa
wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki katika mitandao mbalimbali ya
kijamii kutokana na ajali iliyotokea Arusha na kugharimu maisha ya
wanafunzi, walimu na dereva.
Katika akaunti yake ya Twitter, Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu
ameandika, “Nimesikitishwa na vifo zaidi ya 31 vilivyosababishwa na
ajali mbaya iliyotokea Karatu. Mungu azilaze roho za marehemu mahali
pema.”
Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, ameandika katika ukaunti yake
ya Twitter, “Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na shule ya Lucky
Vincent kwa msiba huu mzito uliopata Taifa letu uliotokana na ajali
mbaya pale Karatu. Tumepoteza watoto wetu ambao wazazi wao, ndugu zao na
Taifa kwa ujumla liliwategema. Kwa kuwa Mungu wetu anaishi na kumiliki
tuendelee kuziombea familia zilizoguswa na msiba huu, watoto wetu
wapumzike kwa amani.”
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, “Moyo wangu umesinyaa baada ya
kusikia taarifa za ajali ya watoto wetu huko Karatu. Natoa salamu zangu
za rambirambi kwa wazazi wa wanafunzi wa shule ya St Lucky kwa ndugu na
familia za walimu na wafanyakazi wa shule waliopoteza maisha.Huu ni
msiba mkubwa sana. Huzuni haielezeki. Nawaombea kwa Mola awape wazazi na
ndugu wote moyo wa subira katika mtihani huu. Ni msiba wa Taifa zima.”