Breaking News

Trump: Kura zinaibiwa vituoni Marekani


Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amedai uchaguzi nchini humo "unaibiwa" na vyombo vya habari pamoja na "kwenye vituo vya kupigia kura" kumzuia kushinda.

Matamshi hayo yanaonekana kukinzana na ya mgombea mwenza wake Mike Pence, ambaye awali aliambia kituo cha runinga cha NBC kwa Bw Trump bila shaka atakubali matokeo ya uchaguzi, licha ya "kuonewa" na vyombo vya habari.

Mshauri wa Bw Trump, Bw Rudy Giuliani pia amewatuhumu wanachama wa Democratic kwa "udanganyifu".

Kura za maoni zinaonesha kwamba Bw Trump anapoteza ushawishi katika majimbo mengi muhimu yanayoshindaniwa.

Hayo yakijiri, mgombea mwenza wa mpinzani wa Trump, mgombea wa chama cha Democratic Bi Hillary Clinton, Bw Tim Kaine amejibu vikali madai hayo ya Bw Trump kwamba kuna njama ya kuiba kura uchaguzini na kusema ni mbinu tu za kutaka kuzua wasiwasi.

Bw trump ametilia shaka uhalali wa shughuli ya sasa ya uchaguzi kwenye msururu wa ujumbe kwenye Twitter.

Ameandika hatimaye kwamba: "Uchaguzi huu bila shaka unaibiwa na wanahabari wasio wa kweli na wa kupotosha ambao wanamtetea Hillary mwovu - lakini pia katika vituo vingi vya kupigia kura - Inasikitisha."

Awali, Bw Trump alikuwa amewatuhumu wanahabari kwa kuchapisha habari za uongo.

"Uchaguzi huu unaibiwa na wanahabari, kwenye juhudi za pamoja wakishirikiana na wanakampeni wa Clinton, kwa kuchapisha habari za mambo ambayo hayajawahi kutokea!"