Breaking News

Serikali yaangamiza ndege aina ya Kweleakwelea waliovamia mashamba ya Mpunga Moshi.




Serikali imeteketeza makundi makubwa ya ndege aina ya Kweleakwelea zaidi ya milioni 3.5 wanaodaiwa kutoka nchi jirani ya Kenya na kuvamia hekta 3725 za Mpunga zilizopo kwenye skimu za umwagiliji za Lower Moshi na Mawala ambazo ni tegemeo kwa chakula nchini.

Mtaalamu wa idara ya maendeleo ya mazao kitengo cha kudhibiti visumbufu vya mimea vinavyohama kutoka wizara ya kilimo mifugo na uvuvi Bw.Gladman Mbokoi amesema zoezi hilo ambalo limeendeshwa na timu ya wataalamu kutokan halimashauri ya wilaya ya Moshi na shirika la nzige wa Jangwani wamefanikiwa kuangamiza ndege hao kwa asilimia 80.

Amesema makundi hayo ya ndege yanadaiwa kutoka nchi jirani ya Kenya na kwamba kwa siku ndege hao wanakadiriwa kuharibu zaidi ya tani 63 za mazao ya nafaka hali ambayo inatishia kuwapo kwa baa la njaa.

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Moshi Bi Butamo Ndalahwa amesema serikali imelazimika kukodi ndege maalumu ya kupulizia sumu kutoka nchi jirani ya Kenya na kutoa sumu lita 325 ambazo zimetumika kuangamiza ndege hao ambao wameharibu vibaya mashamba ya wakulima waishio ukanda wa tambarare.

Naye afisa kilimo na umwagiliaji wilaya ya Moshi Bw.Chikira Mcharo amesema mpaka sasa wamefanikiwa kuokoa hekta 710 za mpunga huku wakulima wakiishukuru serikali kwa zoezi hilo ambalo wanasema mwanzo hali ilikuwa ngumu kwa kuwa walishindwa kudhibiti ndege hao.