TAMKO LA RAIS MAGUFULI JUU YA MIMBA ZA WANAFUNZI LAPINGANA NA SHERIA ZILIZOPO
Tanzania tunayosheria inayoitwa "Statutory Rape"
Sasa hii sheria imewekwa kwa msingi kwamba ukifanya ngono na msichana chini ya miaka 18 - au mwanafunzi kwa ujumla, utakuwa umembaka. Utachukuliwa umembaka kwa kuwa inachukuliwa kwamba katika umri chini ya miaka 18 au kipindi cha uanafunzi, msichana bado ni mtoto na hana akili ya kutambua kwamba kukubali kufanya ngono sio jambo jema. Hivyo huwezi kujitetea kwamba hukumbaka bali mlikubaliana kufanya ngono.
Sasa basi, ikiwa Raisi Magufuli anasema mwanafunzi yeyote akipata mimba asipewe nafasi tena ya kuendelea na shule - kimsingi ni sawa na kusema hakubaliani na sheria ya Statutory Rape.
Kwa maneno mengine - utakuwaje na sheria ya statutory rape - na hapo hapo uamue kwamba mwanafunzi yeyote kupata mimba akiwa shuleni ni uamuzi wake na hivyo moja wapo ya adhabu ni kutompa nafasi ya keundelea na masomo?
Na kumbuka kwamba, kauli ya Raisi Magufuli inadokeza kwamba kila mwanafunzi atakayepata mimba akiwa shuleni kajitakia - yale yale ya kiherehere ya Raisi Kikwete. Hapo hakuna kuangalia sababu wala mazingira ya mimba - awe alibakwa au vinginevyo, mimba ni mimba!
Kwa nini kama Taifa tusijikite katika kuongeza kampeni kuwasaidia hawa watoto kutojiingiza katika ngono za mapema badala ya kutoa adhabu za ujumla zisizoangalia mazingira?
Mie ningemwona Raisi Magufuli ana busara sana kama angesema tutawaruhusu wasome, ila sasa tutatunga sheria atakaempa mimba mwanafunzi afungwe jela maisha! Mimba za wanafunzi zingekoma. Sasa Raisi anaadhibu wanafunzi kuliko wanaowapa mimba!