HII HAPA HISTORIA YA DIKTETA IDDI AMINI WA UGANDA MLA NYAMA ZA WATU......."VERY INTERESTING"
Idi Amin Dada alikuwa mwanajeshi kutoka nchi ya Uganda aliyepindua serikali na kujifanya rais wa Uganda tangu mwaka 1971 hadi 1979 hadi alipofukuzwa na jeshi la Tanzania. Alitawala kidikteta ilhali uchumi wa nchi uliporomoka na makosa mengi ya jinai dhidi ya haki za kibinadamu zilitendwa.
Idadi ya watu waliouawa Uganda kutokana na utawala wake imekadiriwa kuwa kati ya 100,000 na 500,000
Katika miaka yake ya kushika serikali Amin alibadilika kutoka uhusiano wa kirafiki na nchi za magharibi na hasa Israeli kuhamia upande wa Muammar Gaddafi wa Libya, Mobutu Sese Seko wa Zaire, Umoja wa Kisovyeti na Ujerumani ya Mashariki. Hata hivyo Amin alipata usaidizi wa ofisi ya upelelezi ya Marekani CIA iliyotuma silaha na vifaa vingine kwa jeshi lake.
Mwaka 1977 Amin alivunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufalme wa Maungano (Uingereza) akajitangaza kuwa alishinda na kujiongezea sifa ya CBE ("Conqueror of the British Empire"). Kuanzia wakati ule cheo chake rasmi kilikuwa "His Excellency President for Life, Field Marshal Alhaji Dr. Idi Amin Dada, VC, DSO, MC, CBE".
Jaribio la Amin la kutwaa sehemu za Mkoa wa Kagera wa Tanzania kwenye mwaka 1978 lilisababisha Vita ya Kagera baina ya Tanzania na Uganda na mwisho wa utawala wake. Amin alikimbia kukaa ugenini Libya na baadaye Saudia alipoishi hadi kifo chake mwaka 2003.
Alikotoka
Hakuna uhakika juu ya mwaka na mahali alikozaliwa. Amin mwenyewe hakuandika kumbukumbu ya maisha yake wala hakuagiza taarifa rasmi juu ya maisha yake. Vyanzo mbalimbali vinasema ya kwamba alizaliwa mnamo 1925 Koboko au Kampala. Mtafiti Fred Guweddeko amedai Amin alizaliwa 17 Mei 1928, lakini hii imepingwa. Mwanawe Amin Hussein alisema babake alizaliwa Kampala mwaka 1928.
Kufuatana na Fred Guweddeko wa Chuo Kikuu cha Makerere Idi Amin alikuwa mwana wa Andreas Nyabire (1889–1976) wa kabila la Wakakwa, ambaye alikuwa Mkatoliki aliyehamia Uislamu mnamo 1910 akibadilisha jina lake kuwa Amin Dada na kumpa mwana wa kwanza jina hilo pia.
Iddi Amin alilelewa na mama yake bila baba kijijini katika Uganda ya Kaskazini-magharibi. Kufuatana na Gudewekko mamake Amin Assa Aatte (1904–1970) alikuwa Mlugbara aliyetibu watu kwa mitishamba. Amin alisoma miaka kadhaa kwenye shule ya Kiislamu huko Bombo kuanzia mwaka 1941.
Amin mwanajeshi
Baada ya miaka michache ya shule na kazi ndogondogo aliajiriwa mwaka 1946 na afisa Mwingereza wa jeshi la kikoloni King's African Rifles (KAR).
Aliingia jeshini huko Jinja akifanya kazi ya msaidizi jikoni akiendelea kupokea mafunzo ya kijeshi. Baadaye Amin alidai ya kwamba alilazimishwa kuhudumia huko Burma katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mwaka 1947 alihamishiwa Gilgil, Kenya. Mwaka 1949 alitumwa kaskazini kwa kupigania waasi Wasomalia huko. Tangu mwaka 1952 kikosi chake kilihudhuria katika juhudi za kupambana na wanamgambo wa Maumau karibu na Mlima Kenya.
Aliendela kupanda vyeo vilivyopatikana kwa Waafrika katika jeshi la KAR na muda mfupi baada ya uhuru alipewa cheo cha luteni yaani afisa kamili kama mmoja wa Wauganda wawili. Baada ya uhuru wa Uganda mwaka 1962 alikuwa kapteni halafu mwaka 1963 meja. Mwaka 1964 alikuwa makamu wa mkuu na mwaka 1965 mkuu wa jeshi, mwaka 1970 mkuu wa mikono yote ya kijeshi. In 1970, he was promoted to commander of all the armed forces.
Mkuu wa Jeshi na mapinduzi
Amin alipandishwa cheo na waziri mkuu Milton Obote baada ya uasi wa wanajeshi katika Afrika ya Mashariki wa 1964 uliokomeshwa na askari Waingereza katika Tanganyika, Kenya na Uganda akawa makamu wa mkuu wa Jeshi aliyekuwa bado Mwingereza. Kutoka hapa alishirikiana na Obote katika hatua za kuimarisha utawala wa waziri mkuu. Wakati bunge la Uganda lilitaka utafiti kuhusu mashtaka ya Obote kushiriki katika biashara ya siri ya pembe za ndovu kutoka Kongo Obote iliamua kubadilisha katiba na jeshi la Amini lilimfukuza Mkuu wa Dola Kabaka Mutesa kwa nguvu, halafu Obote alijitangaza kuwa rais. Sasa Amin alikuwa kanali na Mkuu wa Jeshi.
Amin alianza kuajiri hasa askari kutoka kaskazini ya Uganda mpakani mwa Sudani.
Mwaka 1970 Obote aliendelea kumpa Amin cheo cha mkuu wa mikono yote ya jeshi na ulinzi. Lakini Amin alisikia pia ya kwamba kulikuwa na mashtaka dhidi yake kutokana na matumizi ya makisio ya jeshi na mipango ya Obote kumfanyia utafiti. Hapo Amin alitumia nafasi ya safari ya Obote kwenda nje kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola, akatwaa mamlaka ya serikali tarehe 25 Januari 1971.
Mtawala wa Uganda
Mwaka 1971 alimpindua rais Milton Obote akajitangaza kuwa rais mpya, lakini wengine hawakumtaka.
Mara moja alianza kuwatesa wafuasi wa Obote na watu wote waliompinga. Kuna makadirio ya kwamba jumla ya watu 100,000 hadi 500,000 waliuawa katika miaka minane ya utawala wake.
Aliharibu uchumi wa Uganda kwa ufisadi na majaribio ya kuongoza biashara. Hatua kubwa ya uharibifu ilikuwa kufukuza watu wote wenye asili ya Kihindi na kugawa maduka na biashara yao kwa ndugu au wafuasi wa rais. Takriban watu 80,000 walipaswa kuondoka kwao wakihamia Uingereza, Marekani au Kanada hasa.
Mnamo Oktoba 1978 Amin alianzisha vita dhidi ya Tanzania kwa kuvamia sehemu za mkoa wa Kagera. Rais Julius Nyerere wa Tanzania aliamua kumwondoa Amin kabisa na jeshi la Tanzania likatwaa Kampala tarehe 11 Aprili 1979.
Amin alitorokea Libya, halafu Irak na mwishowe Saudia alikopewa kimbilio kwa masharti ya kutoshughulikia siasa tena.
Alikufa mjini Jeddah tarehe 16 Agosti 2003.
Je ni Kweli Iddi Amini Alikuwa Akila Nyama za Watu?
Hili bado ni swali ambalo halina majibu, ila watu mbali mbali wamejaribu kuliongelea hili soma hapa chini:
Rais wa Venezuela, Hugo Chavez amewaudhi maafisa wa serikali ya Uganda kwa kauli yake ya kudai kuwa rais wa zamani wa Uganda Idi Amin hakuwa muuaji na mla nyama za watu kama inavyosemekana. Rais wa Venezuela, Hugo Chavez amewaudhi maafisa wa serikali ya Uganda kwa kumtetea rais wa zamani wa Uganda Idi Amin kuwa hakuwa muuaji na mkatili kama inavyojulikana duniani.
"Tulifikiria kuwa Amin ni muuaji mla nyama za watu" Chavez alisema alipokuwa akimuongelea Idi Amin ambaye anatuhumiwa kuwaua mamia ya wapinzani wake wakati wa utawala wake nchini Uganda kwenye miaka ya 1970.
"Nina shaka kama Idi Amin alikuwa muuaji kama inavyosemekana, badala yake alikuwa mwanaharakati mtetezi wa nchi yake", alisema Chavez.
Ingawa hakuna idadi kamili ya watu waliouliwa wakati wa utawala wa Idi Amin kuanzia mwaka 1971-1979, inakadiriwa kuwa watu 500,000 waliuliwa wakati huo.
Mary Karoro Okurut, msemaji wa chama tawala cha Uganda akizungumzia kauli hiyo ya Chavez alisema kuwa mtu yoyote anayedhania kuwa Idi Amin alikuwa ni mtu mwema atakuwa na matatizo ya akili.
"Idi Amin alikuwa ni mtu mkatili ambaye aliua raia wengi wa Uganda na kisha kukimbilia nje ya nchi. Mtu yeyote anayemtetea Amin atakuwa na matatizo".
Naye sekretari wa rais Yoweri Museveni, Tamale Mirundi, alielezea rekodi ya Idi Amin ya kuwaua wapinzani wake akiwemo mmoja wa wake zake.
"Kama unamuoa mwanamke na kisha baadae unamuua, huwezi kuitwa mume mzuri", alisema na kuongeza "Hivyo ndivyo alivyofanya Amin, aliwaua raia wengi wa Uganda hawezi kuitwa mtetezi wa nchi".
Kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusiana na Idi Amin baadhi ya watu wakiamini kuwa ukatili anaotuhumiwa kuufanya zilikuwa ni propaganda za kumchafua huku watu wengi wakiendelea kuamini kuwa Idi Amin ndiye mhusika mkuu kwa mauaji ya watu 500,000.
Miongoni mwa mambo ya kikatili ambayo Idi Amin anatuhumiwa kuyafanya ni kuwaua watu na kula nyama zao na kuhifadhi nyama za watu kwenye majokofu.
Maafisa wa serikali ya Uganda hawajasema chochote kama watachukua hatua zozote za kidiplomasia dhidi ya Venezuela.