Wafanyakazi nchini Uganda wameachwa na mshangao mkubwa baada ya Rais
Yoweri Museveni kukataa kusikiliza kilio chao katika sherehe za
kuadhimisha siku ya Kazi Duniani.
Katika hotuba yake Rais ameonyesha kupuuza ombi la wafanyakazi nchini
la kutaka kuongezewa mishahara kwa kuwa gharama za maisha zimepanda
kutokana na mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa katika sherehe hizo
zilizofanyika Wilaya ya Palisa Mkoa wa Mashariki ya Uganda.
Museveni pia amekaidi msukumo wa vongozi wa wafanyakazi wa kutaka
kiwango cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi kupandishwa kutoka dola
mbili kwa sasa, na badala yake kutaka sheria kuundwa kuwanasa walevi na
wacheza kamari.
Kutokana na kutokuwepo sheria ya kuwabana waajiri wafanyakazi nchini
Uganda wamelalamika kuwa kila mwajiri anakuwa na hiari ya kulipa kiwango
cha mshahara anachotaka.
Viongozi wa wafanyakazi wamesema kuwa sheria iliopo ya mwaka 1984
imeweka kiwango cha chini cha mshahara nchini Uganda kuwa ni Shilingi
6000 ambazo ni chini ya dola 2 za Kimarekani.
Mwenyekiti wa muungano wa wafanyakazi nchini Uganda Wilson Owere
amemlalamikia Rais Yoweri Museveni wakati wa sherehe hizo akisema:
“Haiwezekani kwa binadamu kupokea dola 2 kama mshahara. Zamani walikuwa
wanalipa shilingi za Uganda 6,000 na mpaka leo hivi hakuna kiwango cha
chini.”
“Watu wanawafanyisha kazi wafanyakazi na kuwapa wafanyakazi kile
wanachokitaka kwa sababu hakuna sheria,” amesema mwenyekiti huyo.
Lakini Rais Museveni amewaambia wafanyakazi katika hotuba yake ya
siku ya Wafanyakazi Duniani “adui yenu ni hawa wafanyakazi wa umma ambao
ndio mafisadi wanao wazuilia kupata ajira." “Mimi nalenge kubuni nafasi
za ajira milioni 15,” amesema.
Lakini muungano wa wafanyakazi nchini Uganda wamelaumu sera za
uwekezaji Uganda kwa kuwahusisha wawekezaji kwa vitendo vya dhulma, na
wanawatumikisha wafanyakazi masaa mengi zaidi kuliko vile inavyotakikana
bila `ya malipo yoyote.
“Tukijaribu kuwaunganisha wafanyakazi wawekezaji wanakimbilia kwa rais kulalamika,” wamesema viongozi hao.