Breaking News

Mama Samia Awafuta Machozi Wakunga


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu ameziagiza halmashauri zote nchini kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya hasa maeneo ya vijijini na kipaumbele kitolewe kwa wakunga ambao wanatoa huduma za dharura wajawazito

Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga duniani ambapo amesema kuwa halmashauri zikijenga nyumba karibu na vituo vya kutolewa huduma za afya zitasaidia kupunguza matatizo ya mama na watoto wanaotaka kupata huduma za dharura.

"Baadhi ya watumishi wa afya hasa wakunga wanakaa mbali na maeneo yao ya kazi hivyo utoaji wa huduma za dharura kuwa duni hivyo nawahimiza Wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia ujenzi huo kikamilifu ili kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi nchini"-  Mhe. Samia Suluhu

Akizungumzia Kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini, Makamu wa Rais amewahakikishia wakunga na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini kuwa Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto hizo ikiwemo uboreshaji wa maslahi kwa watumishi wa kada hiyo pamoja na kuongeza maradufu vifaa tiba,dawa na vitendanishi ili kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata huduma bora za afya.

Makamu wa Rais pia amewahimiza wakunga kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia maadili na waache tabia ya kutoa lugha mbaya kwa wanawake wajawazito na wakunga watakaobainika kufanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo.

Kauli mbinu ya maadhimisho ya Siku ya Wakunga mwaka huu ni Wakunga,Akina mama na Familia ni washirika wa Kudumu.(Midwives,Women and Families Partners)