GWAJIMA AMKINGIA KIFUA LOWASSA...AMVAA ALIYETABIRI CHA LOWASSA.

Katika
moja kati ya mahubiri yake, Nabii Bushiri ambaye ni mzaliwa wa Malawi
anayefanya kazi zake nchini Afrika Kusini, alidai kuwa ameona hali ya
umauti ikimnyemelea Lowassa na kuwataka waumini wake kuomba ili awe na
maisha marefu.
Akizungumzajana Jumapili katika ibada kanisani kwake, Gwajima alilaani utabiri wa Nabii
Bushiri, akidai kuwa amekodiwa na watu wenye nia mbaya ili atabiri ubaya
kuhusu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ili kufanikisha mpango wao
wa kufanya tukio baya.
Gwajima
alidai kuwa kwa uwezo wa kiroho, amewafahamu watu waliopanga kutekeleza
njama dhidi ya Lowassa na viongozi wengine wa Serikali huku wakimtumia
nabii huyo kuwaandaa watu kisaikolojia.
“Nataka
nimueleze Nabii Bushiri kuwa nafahamu watu waliomkodi kufanya hivyo, na
utabiri wake hautawezekana kamwe. Hakuna kiongozi yoyote wa serikali
wala wa upinzani atakayekufa kwa utabiri huo. Wote wataishi kwa jina la
Yesu,” alisema Gwajima ambaye jana alikuwa akihubiri kwa lugha ya kiingereza na kufasiriwa kwa lugha ya kiswahili.
Hata
hivyo, Askofu huyo anayefahamika kwa kauli zake tata alieleza kuwa kwa
uwezo wa kiroho amewafahamu watu waliopanga njama hizo na namna
walivyoenda Afrika Kusini kukutana na mhubiri huyo kwa lengo la kumkodi
atoe utabiri huo.
“Wanaweza
kujiuliza nimewafahamu vipi. Roho yangu ilisafiri nao hadi Afrika
Kusini, walivyokutana na Nabii Bashiri nilikuwa naye, yote
waliyozungumza naye nayafahamu na hata walichompa ninakifahamu,” alisema.
“Ninawafahamu
kwa majina na walipo na ninawataka wakome mara moja kuendelea na mpango
wao. Wasipositisha mpango wao huo, Jumapili ijayo nitawataja hapa wote
kwa majina,” alisikika Gwajima.
Gwajima
alidai kuwa hamaanishi kuwa Bushiri sio mtumishi wa Mungu, lakini
utabiri wake juu ya viongozi wa Tanzania ni wa kukodiwa.
Nabii
Bushiri ambaye amekuwa akizua mijadala na hata kuingia katika mgogoro
na baadhi ya nchi za Afrika, pia aliwahi kutabiri kuhusu matokeo ya
uchaguzi mkuu Tanzania pamoja na tukio la tetemeko la ardhi nchini.


