CHADEMA USO KWA USO NA CCM DODOMA, WAPANGA KUTETA HAYA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kukutana mjini
Dodoma kwa lengo la kufanya mijadala kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi
nchini.
Chama hicho kimepanga kufanya mikutano yote ya Baraza Kuu, Sekretarieti
na Mkutano wa Kamati Kuu mjini hapo mwishoni mwa mwezi huu ikiwa ni mara
ya kwanza kwa chama hicho kikuu cha upinzani kukutana katika mji huo
ambao ni ngome ya CCM na pia makao makuu ya nchi.
Kwa mujibu wa mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene, mikutano hiyo itaanza Mei 28.
“Baada ya kikao cha Baraza Kuu, sekretarieti ya Chama Makao Makuu
itaketi Mei 28 na kisha Kamati Kuu nayo itaketi Mei 29,” Makene
anakaririwa na Mwananchi.
Makene alieleza kuwa wameamua kufanyia mkutano huo Dodoma ambayo ni
Kanda ya Kati ya chama hicho inayojumuisha mikoa ya Singida na Morogoro
ikiwa ni sehemu ya uamuzi wake wa kuzipa nafasi kanda kuandaa mikutano
mikuu.
Kamati Kuu ya Chadema inaketi mjini Dodoma ikiwa ni miezi miwili tu
baada ya Kamati Kuu ya CCM kukutana mjini humo ambapo ni makao makuu ya
chama hicho tawala.