Breaking News

MWANAFUZI WA KIDATO CHA NNE APANDISHWA KIZIMBANI KWA UHALIFU WA KUTUMIA BASTOLA



Mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya Sekondari Njechele wilayani Kinondoni, Salum Daudi (18) ni miongoni mwa washtakiwa watatu waliopandishwa kizimbani jana kwa kosa la kufanya uhalifu kwa kutumia bastola.

Daudi, pamoja na washtakiwa wengine; Peter Onesmo (23), Yohana Peter maarufu Kube (27) na Juma Hemed (22) walipandishwa jana katika mahakama ya Hakimu Mkazi, Kinondoni kwa kosa la kupora Sh1 milioni kwa kutumia bastola na panga katika tukio hilo.

Wakili wa Serikali, Grace Lwila akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina, alidai washtakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 9 eneo la Madale, jijini Dar es Salaam.

Katika hati ya mashtaka, Lwila alidai kuwa vitu vingine vilivyoporwa katika tukio hilo ni pamoja na vocha, simu mbili ambazo washtakiwa hao wanazitumia.

Mahakama hiyo ilielezwa kuwa simu hizo ni mali ya Meshack Costantino.

Lwila alidai kuwa washtakiwa hao kabla ya kutenda kosa hilo walimtishia Hillary Justine na Samwel Leonard kwa silaha, wakiwa nyumbani kwao ili waweze kujipatia mali hizo jambo ambacho ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao walikana kosa na upande wa Jamhuri uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa sababu upelelezi unaendelea.

Hakimu Mhina alisema shtaka hilo halina dhamana, hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 6 itakapotajwa tena.