POLISI WAZINGIRA MGODI WA BULYANHULU
Jeshi la Polisi limeuzingira mgodi wa Bulyanhulu baada ya Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga, Zainab Tellaack kuzuiwa kuingia katika mgodi huo
alikokwenda kukagua iwapo uzalishaji unaendelea bila kuwepo kwa Maofisa
wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA).
Jeshi hilo limefanya hivyo baada ya Tellack kuagiza kuimarisha ulinzi
katika eneo lote la mgodi huo kuhakikisha hakuna mtu anyetoka wala
kuingia.
Mapema jana Alhamisi, Mkuu huyo wa mkoa alitembelea mgodi mwingine wa Buzwagi
ambao pia unamilikiwa na kampuni ya Acacia kama ulivyo ule wa
Bulyanhulu.
Katika mgodi wa Buzwagi, Tellack na msafara wake waliruhusiwa kuingia na
kushuhudia shughuli za uchimbaji ukiwa umesitishwa kwa kukosekana
maofisa wa TMAA walioondoka mara baada ya Rais Magufuli kutangaza
kuvunja bodi na kutengua uteuzi wa watendaji wakuu wa wakala hiyo.