Muigizaji mkongwe nchini Jacob Stephen 'JB amefunguka na kudai
hawakufanya maandamano ya kuzuia movie za nje ya nchi kuuzwa nchini bali
waliandamana kuzitaka zilipiwe kodi au serikali itoe msamaha kwenye
filamu za ndani.
JB amezungumza hayo alipokuwa akifanya mahojiano na wanahabari wakati wa
uzinduzi wa filamu ya Tunu na kudai kuwa watu wengi wamehusisha
maandamano yao na siasa kitu ambacho hakina ukweli na kuongeza kuwa
tasnia ya filamu kwa sasa inahitaji watu watakaowasaidia kumaliza kilio
chao. "Sisi hatupingi movie za nje kuingia nchini, mimi mwenyewe
nazipenda na ninaziangalia. Hapa ugomvi uliopo ni wao watozwe kodi au na
sisi tuondolewe hizo kodi, wakifanya hivyo hakuna mtu ambaye atapiga
kelele tena. Sasa hivi nakatwa asilimia 30 lakini bado natakiwa nitoe
asilimia tano na wakati huo huo, nikitaka kutoa movie mpaka nikaombe
kibali kama ni wewe ungekubali? Na jambo hili lisihusishwe na siasa
kwani sisi mtu yoyote ambaye ataweza kutusaidia kutusemea tutamsikiliza
hata akiwa wa upinzani hatuna shida" Alisema JB
Aidha msanii huyo ameongeza kuwa wasanii wenzao wanaowakejeli kwa
kuandamana wengi wao hawategemei movie kuwaingizia kipato na ndio maana
wanaongea maneno ya ajabu huko nje. "Msanii yoyote ambaye filamu ndiyo
chakula chake hawezi kuwa nje ya hili kwa sababu hataweza kuishi. Mimi
niseme tu siwezi kuishi bila filamu ndiyo maana tunapiga kelele. Sitaki
kuwataja majina lakini angalia tu wewe mwenyewe huyo mtu ambaye hataki
kupiga kelele anaishi bila filamu?" JB alimaliza