Tofauti na vyakula vingine, ndizi zina faida kubwa sana katika mwili wa
binadamu. Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, ndizi zina virutubisho vya
aina mbalimbali kama vile, protini, mafuta, kalishiamu, wanga,
fosiforas, madini ya chuma, vitamin A,B,C na maji.
Ndizi zina faida zipi katika urembo? Chanzo cha nishati Ndizi zina uwezo
wa kumeng’enywa kwa urahisi zaidi, tena zina nishati kubwa, sukari
iliyomo katika ndizi ni chanzo kizuri sana cha nishati.
Hivyo naweza kusema kuwa ndizi ikiliwa ipasavyo itakusaidia kujenga
mwili na misuli yako kwa ujumla. Husaidia kuondoa chunusi Chunusi ni
miongoni mwa matatizo ambayo huwasumbua warembo wengi hususan wanawake.
Je, unafahamu kuwa ndizi mbivu zinaweza kukuondolea tatizo hilo? Kwa
kuchanganya ndizi mbivu na maziwa na asali na kisha kuzisaga ili kupata
urojo ambao utatumia kupaka kwenye maeneo yaliyoathirika, unaweza
kuondokana kabisa na tatizo hilo.
Fanya hivyo kila siku na hakikisha unakaa na mchanganyiko huo kwa muda
usiopungua dakika 30 hadi 40, kisha osha na maji ya baridi ikiwezekana
yaliyopozwa na jokofu.
Ndizi katika ‘diet’ Ndizi zina nafasi kubwa sana kati kuongeza au
kupunguza uzito, hivyo unaweza kutumia ikiwa unahitaji kupunguza ama
kuongeza uzito wako.
Kwa wajawazito Ndizi ni chakula kizuri kwa wanawake wajawazito, kwani
kina kiwango kikubwa cha ‘folic acid’ ambayo inaweza kufyonzwa kwa
urahisi sana na kiumbe kilicho tumboni. Ikiwa mama mjamzito atatumia
ndizi mara kwa mara ni wazi kuwa atakuwa mwenye muonekano mzuri na wa
kuvutia.
Ni kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, presha, vidonda vya tumbo, saratani ya figo, kukosa choo
Ndizi mbivu ni tunda ambalo linafahamika na kila mtu, lakini sina hakika
kama watu wengi wanafahamu umuhimu na faida za tunda hili ambalo
linapatikana kirahisi sana nchini. Bei yake ni kati ya shilingi 50 na
150 tu, kiwango cha pesa ambacho kila mtu anaweza kukimudu.
Iwapo ulikuwa hujui umuhimu wa kula ndizi mbivu, leo utalazimika
kubadili mtizamo wako na kuziangalia ndizi kama tunda muhimu katika
kuupa nguvu na kuulinda mwili wako dhidi ya maradhi hatari ambayo hayana
tiba. Watu wa michezo pia wanapaswa kuliona tunda hili kuwa ni muhimu
sana katika kuipa miili yao nguvu.
KINGA DHIDI YA SHINIKIZO LA DAMU NA MARADHI YA MOYO
Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi, ndizi ni chanzo kikubwa cha
Potassium, madini ambayo ni muhimu sana katika kuweka shinikizo la damu
mwilini katika hali yake ya kawaida (Normal Blood Pressure), na ufanyaji
kazi mzuri wa moyo. Kwa kuwa ndizi moja ina wastani wa 467mg za madini
aina ya Potasiamu na 1mg ya sodiamu (chumvi), ndizi moja tu kwa siku
inaweza kukupa kinga ya maradhi ya shinikizo la damu na matatizo ya
moyo.
Ukweli kuhusu vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya Potasiamu
katika kushusha shinikizo la damu mwilini, umethibitishwa na tafiti
nyingi za kisayansi. Kwa mujibu wa jarida moja la masuala ya afya nchini
Marekani, zaidi ya Wamarekani 40,000 wa kike na kiume, walifanyiwa
utafiti kwa muda wa miaka minne na ikagundulika kwamba watu wanaokula
vyakula vyenye kiasi kikubwa cha madini ya Potasiamu na kirutubisho cha
Fiber (Ufumwele), wako katika hatari ndogo ya kupatwa na kiharusi.
Aidha, utafiti mwingine uliofanywa na taasisi moja ya masuala ya tiba
ijulikanayo kama Archives of Internal Medicine, ya nchini Marekani, pia
ilithibitisha kwamba ulaji wa vyakula vyenye kiasi kikubwa cha ufumwele
(fiber) kama vile ndizi, husaidia sana kutoa kinga dhidi ya maradhi ya
moyo. Na katika suala hili, zaidi ya watu 10,000 walifanyiwa utafiti kwa
muda wa miaka 19.
KINGA DHIDI Y VIDONDA VYA TUMBO
Kwa muda mrefu sana imethibitishwa kwamba ndizi ina virutubisho vyenye
uwezo wa kupambana na asidi tumboni hivyo kutoa kinga dhidi ya vidonda
vya tumbo (stomach Ulsers) na kutoa ahueni kwa mtu ambaye tayari
ameathirika. Katika utafiti mmoja, ilkibainika kwamba mtu akila
mchangayiko wa ndizi mbivu na maziwa freshi, huzuia utokaji wa asidi
tumboni inayosababisha vidonda vya tumbo.
Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi juu ya suala hili, ndizi hutoa kinga
na ahueni ya vidonda vya tumbo kwa njia mbili. Mosi: virutubisho
vilivyomo kwenye ndizi huzipa uhai seli zenye kazi ya kutengeneza utandu
ambao hutoa aina fulani ya urojo (mucus) unaotumika kama kizuizi dhidi
ya asidi tumboni.
Pili: kuna virutubisho vingine kwenye ndizi ambavyo kwa kitaalamu
vinajulikana kama ‘Protease’ ambavyo husaidia kuondoa bakteria tumboni
ambao wanaelezewa kuwa ndiyo chanzo cha vidonda vya tumbo. Hivyo kama
wewe hujaptwa na vidonda vya tumbo, kwa kula ndizi mara kwa mara unajipa
kinga madhubuti na kama tayari umeathirika na vidonda, kwa kula ndizi
utajipa ahueni kubwa.
NDIZI KAMA TIBA KWA WENYE MATATIZO YA CHOO
Ndizi ni muhimu sana katika kulainisha na kusafisha tumbo na kumuwezesha
mtu kupata choo. Mbali ya kusaidia upatikanaji wa choo kwa wenye
matatizo hayo, lakini pia hutoa ahueni kwa wagonjwa wa kipindupindu. Mtu
aliyepatwa na kipindupindu hupoteza kiasi kikubwa cha madini ya
Potasiamu, hivyo kwa kula ndizi ataweza kurejesha mwilini maidni yake
yaliyopotea na kuupa mwili nguvu yake.
UIMARISHAJI WA NURU YA MACHO
Wakati ulipokuwa mdogo, bila shaka uliwahi kuambiwa na mama kuwa mtu
akila karoti, atakuwa akiona vizuri. Bila shaka hakukosea, lakini sasa
ukiwa mtu mzima unaambiwa kwamba ulaji wa matunda, ikiwemo ndizi, ndiyo
kinga hasa dhidi ya matatizo ya kutokuona vizuri uzeeni. Utafiti wa hivi
karibuni unaonesha kwamba ulaji wa matunda kwa wingi kila siku,
hupunguza kwa asilimia 36 matatizo ya kutokuona vizuri kutokana na mtu
kuwa na umri mkubwa.
KINGA DHIDI YA SARATANI YA FIGO
Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na Jarida la Kimataifa la masuala
ya Saratani (International Journal of Cancer) la nchini Marekani,
umeonesha kwamba ulaji wa mara kwa mara wa matunda halisi, hasa ndizi
mbivu, ni kinga madhubuti ya mwili. Zaidi ya wawake 50,000 wenye umri
kati ya miaka 40 na 76 waliofanyiwa utafiti, ulionesha kuwa wale
waliokula wastani wa milo 2.5 ya matunda na mboga kila siku, walipunguza
hatari ya kupatwa na saratani ya figo kwa asilimia 40.
Baadhi ya vitamini na madini yaliyomo kwenye ndizi ni pamoja na Vitamini
B6, Vitamin C, Potassium, Dietary Fibre na Mnganese. Hivyo utaona
kwamba tunda la ndizi ni muhimu kwa sababu limesheheni vitamini na
madini muhimu katika mwili wa binadamu. Kuanzia leo itazame ndizi kama
tunda muhimu sana katika ustawi wa afya yako na ni kinga dhidi ya
maradhi unayoweza kuyaepuka kesho kwa kula tunda hili kwa wingi leo!
Hizi hapa faida za ndizi katika mwili wa binadamu!
Reviewed by Mipiko
on
6:54 PM
Rating: 5