Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita
Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia mwanamume mmoja
Severini Elius(57), mkazi wa Kijiji cha Mabogini wilayani Moshi mkoani
Kilimanjaro kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka minne.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani
hapa, Koka Moita, alisema tukio hilo lilitokea Desemba Mosi mwaka huu
saa 10 jioni, katika Kijiji cha Mabogini kata ya Mabogini wilayani humo.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mfugaji anadaiwa kumbaka mtoto huyo na
kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri ambapo tukio
hilo lilibainiwa na dada wa mtoto huyo.
“Beatrice George (17) mwanafunzi na mkazi wa mabogini alibaini kubakwa
kwa mdogo wake ambapo mzee huyo alimkuta mtoto akiwa nyumbani kwao peke
yake akamvamia na kumvutia chumbani na kisha kuanza kumbaka kwa nguvu.
“Baada ya dada yake kurejea nyumbani alimkuta mdogo wake akiwa analia
huku akilalamika kwamba ana maumivu makali sehemu zake za siri huku
akiwa anamtaja mzee huyo ambapo baada ya yeye kumchunguza alibaini kuwa
amebakwa na kuja kutoa taarifa polisi,” alisema.