KABLA ya kuamua kuwa Mjasiriamali ni vyema ukakaa chini na kujichunguza
mwenyewe kama kweli unaweza kuwa Mjasiriamali kwa kujiajiri mwenyewe.
Kama unajiona unaweza kuwa Mjasiriamali, basi hatua zifuatazo
unazoletewa hapa zinaweza kukusaidia sana kuwa Mjasiriamali mwenye mafanikio kama utathubutu kuchukua hatua.
Watu wengi wana mawazo mazuri ya kufanya biashara ambayo yanaweza
kubadili hali zao za kiuchumi na hata kuwatajirisha, lakini bado
hawajaamua kuchukua hatua kuyafanyia kazi mawazo yao yawazalishie fedha.
Uchaguzi Sahihi
Kuamua kuwa mjasiriamali ni suala linalohitaji maamuzi ya hali ya juu
kwa kuwa ni uchaguzi wa maisha yako. Jiangalie mwenyewe kama uko tayari
kwa wewe mwenyewe kuwa bosi na kiongozi wa biashara yako. Ukikubali
kubeba jukumu hilo, lazima sasa ukubali kuchukua jukumu la maisha yako
kwa asilimia zote.
Ni vyema ukajichunguza na kujitathmini kama una tabia ambazo
zitakukwamisha, ukashindwa kujiajiri kwa maana suala la kujiajiri si
suala tu la kuwa na fedha ama mtaji. Kama wewe huwezi kujisimamia, ni
mtu wa kuambiwa kila kitu cha kufanya au kitu cha kuacha kufanya. Kama
wewe ni mwoga wa kuthubutu, ni mvivu au mzembe, na unafikiri mafanikio
ni kitu rahisi na jambo la mkato tu, basi kazi ya Ujasiriamali siyo
yako, huiwezi.
Katika dunia ya leo hakuna kitu rahisi. Kila jambo lina ugumu wake,
lina vikwazo ambavyo unatakiwa uvivuke ndipo uyafikie mafanikio au
kuingia katika hatua nyingine ya kiuchumi.
Yako mambo muhimu ambayo kama Mjasiriamali unapaswa kujitathmini juu ya
nguvu uliyonayo na udhaifu ulionao utakusaidia kupiga hatua kwa kujua
kitu gani unacho na kipi unahitaji na wapi unahitaji kufika kibiashara
au kiuchumi.
Kujitambua Uwezo na Udhaifu
Kila mtu anayetaka kuingia kwenye Ujasiriamali, anapaswa kutafuta muda
binafsi wa kujitathimini juu ya Uwezo na Udhaifu wake. Lazima ujue ni
nini unaweza kufanya vizuri sana, na nini hauwezi.
Hii itakiusaidia kuchagua aina ya biashara unayoiweza kwa urahisi sana.
Hii itakuwa pia fursa ya kujifunza na kuwa bora zaidi katika kile
ulichochagua kufanya. Kwa mfano, ili uwe Mjasiriamali mahiri katika eneo
ulilolichagua, lazima ujue kwamba wewe unajua nini. Kama ni mpishi
mzuri, basi chagua upishi. Kama ni mchoraji mzuri, basi chagua uchoraji.
Kwa kufanya hivyo, hiyo itakuwa rahisi kuyafikia mafanikio
unayoyatarajia.
Una Mafunzo Yoyote?
Kusoma na kujifunza kila siku ni kiungo muhimu sana. Mjasiriamali
lazima awe na taaluma, elimu au uzoefu wa biashara anayotaka kuifanya.
Duniani kote kuna elimu za aina mbili. Elimu rasmi na elimu isiyo
rasmi. Zote hizi ni elimu zinazomsaidia Mjasiriamali kufikia malengo
yake, iwe ni kwa kuhudhuria mafunzo tofauti tofauti ya Ujasiriamali au
kwa kujifunza peke yake katika eneo lake la kazi, hata kama ni kwa
gharama kubwa kiasi gani. Lengo ni kuwa bora katika kile unachofanya au
unachotarajia kufanya.
Kuyafahamu Mazingira na Kuyamudu
Kwa kuyatambua mazingira yanayokuzunguka na kuweza kuyamudu, kunamfanya
Mjasiriamali kutambua fursa zilizo katika eneo lake, na pia inakuwa
rahisi kutengeneza biashara itakayoendana na mazingira hayo. Hata hivyo,
ni lazima ufanyike utafiti wa kutosha katika mazingira hayo kuhusu
biashara au huduma inayopaswa kufanyika.
Aina ya Bidhaa/Huduma
Mjasiriamali akishayafahamu mazingira, ni vyema sasa akafanya utafiti
wa kutosha kutambua ni bidhaa za aina gani au huduma ambayo wateja wake
watahitaji. Ni wakati sahihi kwa Mjasiriamali kuanza kutoa huduma na
kufanya biashara mara moja bila kuchelewa.
Sajili Biashara/Huduma yako
Kwa wakati tunaoishi kwa sasa, ambao ni wa sayansi na teknolojia,
inatakiwa tufanye mambo kisasa. Kama umeamua kuwa Mjasiriamali ni vyema
kutafuta vielelezo vya kisheria vitakavyokulinda wewe na biashara yako.
Kwa hiyo, kitu muhimu hapa ni kusajiri kampuni yako binafsi au hata
jina la biashara yako tu ili iweze kutambulika kisheria. Ukishasajiri
utapatiwa namba ya utambulisho wa Mlipakodi (Tin Number) na
leseni ya biashara yako.Vielelezo hivi vitakufanya ufanye biashara yako
kwa wigo mpana zaidi na pia itakuwa ni rahisi kupata mikopo.
Boresha Mawasiliano na Wateja
Kwa wakati huu wa ushindani mkubwa wa kibiashara, ni vyema kufanya
shughuli zako kwa ufanisi mkubwa. Tafuta vielelezo vitakavyoonyesha
taarifa za biashara au huduma yako. Jitambulishe wewe mwenyewe ni nani,
unapatikana wapi na unafanya nini.
Hii ni njia rahisi sana ya kujitangaza. Kama Mjasiriamali, kuwasiliana
na watu wanaokuzunguka ni suala la muhimu sana katika kukuza biashara
yako, kwa maana hao ndio wateja wako.
Aidha, unaweza kutumia vyombo vya habari kujitangaza ili kuwavutia
wateja wapya na kujitengenezea mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Kwa mfano tunaona makampuni ya soda yamekuwepo kwa miaka mingi, lakini
bado hadi sasa yanaendelea kujitangaza na kujijengea mvuto kwa wateja
wake na wateja wapya kujivunia bidhaa zao na kujiamini pale
wanapozitumia.
Kwa hiyo, kwa Mjasiriamali, kujitangaza ni suala muhimu sana hasa
katika dunia ya sasa ya utandawazi. Katika kujitangaza huko, unaweza
kutumia hata mitandao ya kijamii kama vile Facebook, JamiiForums, Twitter, Instagram na WhatsApp na mingine mingi.