Mbunge Wa Ukonga "CHADEMA" Atiwa Mbaroni

Mbunge
wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa
wa Temeke kwa tuhuma ambazo hazikuweza kujulikana mara moja.
Taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo, zilianza kusambaa jana jioni, huku zikimuhusisha na mgogoro wa ardhi.
Katibu
wa mbunge huyo, Deogratius Salit jana alikiri Waitara kukamatwa na
polisi wakati wa ubomoaji wa nyumba za wakazi wa Kata ya Kivule.
Salit
alisema nyumba hizo zilibomolewa baada ya kuwapo kwa mgogoro baina ya
wananchi wa kata hiyo na Kikundi cha Umoja wa Vijana wa Kikristo
Tanzania (UVIKITA) kinachodaiwa kumili eneo hilo licha ya wananchi hao
kushinda kesi mahakamani.
Alisema
mbunge alifika kwenye eneo hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa
wananchi kwamba nyumba zao zinabomolewa na Jeshi la Polisi.
“Mbunge
alifika katika eneo hilo baada ya kupata taarifa ya kuwapo kwa ubomoaji
katika Kata ya Kivule na alifika pale kwa sababu yeye pia ni mwenyekiti
wa kata hiyo.
“Baada
ya kufika pale alikuta askari wakisimamia ubomoaji huku wakirusha
mabomu ya machozi na kuwatawanya wananchi, aliwauliza askari kama wana
nyaraka zozote za kuvunja nyumba hizo, ndipo walimwambia kuwa nyaraka
hizo zipo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Chang’ombe” alisema.
Salit
alisema wakati wakiwa njiani kuelekea Polisi Chang’ombe, Waitara
aliwataarifu kwamba amekamatwa na kupelekwa katika kituo hicho.
Alisema
hadi sasa bado hawajajua sababu za kukamatwa kwa mbunge huyo na
wanamsubiri wakili wake aitwaye Hekima kwa mahojiano zaidi.
Salit alisema zaidi ya nyumba 200 zimebomelewa na kuwaacha wananchi wa eneo hilo wakiwa hawana mahali pa kuishi.


