Breaking News

CHINA NA RUSSIA ZIMETANGAZA KUPINGA UTUMIAJI NJIA ZA KIJESHI DHIDI YA KOREA KASKAZINI


Mwakilishi wa Uchina katika Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba Beijing inapinga aina yoyote ya utumiwaji njia za kijeshi kuhusiana na Korea Kaskazini. Kadhalika Liu Jieyi ametaka kusitishwa hatua ya Marekani ya kuweka ngao ya makombora aina ya THAAD katika ardhi ya Korea Kusini.

Kabla ya hapo pia, mwakilishi wa Uchina katika Umoja wa Mataifa alinukuliwa akisema kuwa, endapo migogoro itaendelea kushuhudiwa katika eneo la Peninsula ya Korea na kuharibu usalama wake, basi haraka sana dunia itashuhudia msiba mkubwa. Naye kwa upande wake, Pyotr Ilyich, naibu mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, ni lazima Marekani isitishe hatua ya uwekaji ngao yake ya makombora nchini Korea Kusini, kama ambavyo inatakiwa pia kusimamisha utumiwaji wa njia yoyote ya kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini.

Hii ni katika hali ambayo Jumanne iliyopita, Rais Donald Trump wa Marekani aliitaka Uchina kuchukua uamuzi mgumu kuhusiana na hatua ya Pyongyang ya kuvurumisha kombora jipya la balestiki ambalo lina uwezo wa kushambulia ardhi ya Marekani. Jumanne asubuhi Korea Kaskazini ilivurumisha kombora jipya la balestiki kutoka  ardhi yake iliyo karibu na mpaka wa Uchina kuelekea bahari ya Japan.