MWANZA:BINTI WA MIAKA 15 ABAKWA NA VIJANA WANNE
Watu
watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi huku mwingine mmoja akiendelea
kutafutwa kwa tuhuma za kumbaka binti mmoja mwenye umri wa miaka 15
wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Akitoa
taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amesema
kwamba tukio hilo limetokea tarehe 21/05/2017 majira ya saa moja kamili
jioni katika maeneo ya mamlaka ya pamba, kata ya Kirumba ambapo inadaiwa
kuwa binti huyo ambaye pia ni mkazi wa Kirumba alikuwa na mahusiano ya
kimapenzi na mtuhumiwa aliyejulikana kwa jina moja la Phili na walipanga
wakutane katika maeneo hayo.
Inasemekana
kuwa binti huyo alikutana na mpenzi wake mahali hapo kisha walikwenda
sehemu yenye jumba bovu kuzungumza, wakiwa kwenye eneo hilo ghafla
walitokea vijana wengine watatu wakishirikiana na Phili na kuanza
kumfanyia ukatili kwa kumbaka.
Inasemekana
kuwa wakati wakiendelea na ukatili huo binti alipiga yowe akiomba
msaada kutoka kwa wananchi, wananchi walifika eneo la tukio na kumuokoa
binti na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Fredy Remigius
kisha walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo.
Askari
walifika katika eneo la tukio na kufanya msako mkali wa kuwatafuta
watuhumiwa wengine huku wakishirikiana na wananchi na kufanikiwa
kuwakamata watuhumiwa wengine wawili huku mmoja aliyekuwa na mahusiano
ya kimapenzi na binti akifanikiwa kutoroka.
Amewataja
watuhumiwa hao kuwa ni Fredy Remigius miaka 20, mkazi wa Kitangiri,
Jackson Joseph miaka 17, mkazi wa Mlimani B na Frank Haruni miaka 18.
Kamanda
Msangi amesema mahojiano na watuhumiwa waliokamatwa yanaendelea na
pindi uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani na kwamba majeruhi
aliyebakwa amepelekwa hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa ajili
ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri.