ALIYEKUWA RAIS WA KOREA KUSINI AMEFIKISHWA MAHAKAMANI KUJIBU TUHUMA ZINAZOMKABILI
Aliyekuwa
Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amefikishwa mahakamani kwa mara ya
kwanza kujibu mashtaka yanayomkabili, tangu alipokamatwa mwezi Machi
mwaka huu.
Mwanasiasa
huyo aliyeondolewa madarakani kwa kashfa nzito, anakabiliwa na mashtaka
kadhaa ikiwa ni pamoja na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na
kuvujisha siri za Serikali. Hata hivyo, Park aliyefikishwa mahakamani
hapo na gari la magereza akiwa amefungwa pingu mikononi alikana mashtaka
yote dhidi yake.
Park
anatuhumiwa kushirikiana na rafiki yake, Choi Sonn-sil, kuchota fedha
kinyume cha sheria kutoka kwa makampuni makubwa ya nchi hiyo ikiwa ni
pamoja na kampuni ya Samsung, kwa malengo ya kupata mrejesho wa faida ya
kisiasa.
Choi
Soon-sil ambaye pia anakabiliwa na mashtaka alifikishwa mahakamani
pamoja na mwanasiasa huyo lakini pia alikana mashtaka yote dhidi yake.
Kiwango cha juu zaidi cha adhabu kwa kosa la kupokea au kutoa rushwa nchini Korea Kusini ni kifungo cha maisha jela.