HANS POPPE AELEZA SABABU YA YEYE KUJIUZULU UONGOZI WA SIMBA SC.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema
kwamba ameamua kujitoa kwenye uongozi wa klabu hiyo kuepuka kuwa sehemu ya
watu wasio waungwana.
Hans Poppe amesema kwamba uongozi wa
Simba chini ya Rais wake, Evans Elieza Aveva umemfanyia mambo yasiyo ya
kiungwana, mwanachama Mohammed ‘Mo’ Dewji.
Hans Poppe amejiuzulu Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba na maana
yake amejivua pia na uongozi wa Kamati ya Usajili na ya ujenzi wa Bunju
Complex baada ya kuchukizwa na kutohusishwa katika mkataba wa udhamini
wa kampuni ya SportPesa.

Zacharia Hans Poppe (kulia) amesema hataki kuwa sehemu ya watu wasio waungwana Simba
“Siyo kushirikishwa mimi tu, bali Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji
pia, lakini kubwa zaidi tuna makubaliano na Mo (Dewji) kuwa tukitaka
kuingia mkataba na yeyote Yule, hakatai lakini tumshirikishe, sasa
tunasaini mkataba kwa kumzunguka ni kukosa uungwana na siwezi kuwa
sehemu ya hilo,”amesema.
Poppe amesema kwamba alijaribu sana kutaka kukutana na viongozi wa Simba
kujadili nao suala hilo, lakini walikuwa wanamkwepa ndiyo maana ameamua
kujiuzulu; “Hatujakaa, kila nikiwaambia tulijadili wanaingilia huku
wanatokea kule,”.

Dewji anayetaka kununua hisa Simba, amesikitishwa na uongozi wa klabu
hiyo kwa kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila
kumshirikisha.
Na habari ambazo hazijathibitishwa na upande wowote, zinasema Mo Dewji,
Mbunge wa zamani wa Singida Mjini ameuandikia barua uongozi wa klabu
hiyo chini ya Rais wake, Evans Aveva kudai alipwe fedha zake, Sh Bilioni
1.4 alizokuwa anaikopesha Simba kwa kulipa mishahara ya wachezaji na
benchi la Ufundi, Sh Milioni 80 kila mwezi.
Imedaiwa Mo Dewji alikuwa anatoa fedha hizo kwa makubaliano zitalipwa
wakati mpango wake wa kununua hisa za klabu utakapokamilika. Mo
alikubaliana na uongozi wa Simba kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh.
Bilioni 20 mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba
utakapokamilika.
Lakini zoezi hilo linaelekea kuingia doa baada ya Mo Dewji kuandika
katika ukurasa wake wa Twitter akilalamikia uongozi wa klabu kuingia
mkataba na SportPesa bila kumshirikisha.
Na upande mwingine, uongozi wa Simba na umemeguka baada ya Hans Poppe
naye kuandika barua ya kujiuzulu, naye pia akilalamikia kutoshirikishwa
katika mkataba wa SportPesa.


