Breaking News

Vyama 10 vya upinzani vyatinga Mahakamani kupinga muswada wa vyama vya siasa (+video)

Umoja wa vyama 10 vya  upinzani nchini Tanzania umefungua kesi Mahakamani Kuu ya Tanzania kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa kujadiliwa na Bunge kwa ajili ya kuupitishwa kuwa sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya tamko hilo, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema muswada huo unakinzana na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 hivyo ni muhimu kwao kuupinga. SOMA TAARIFA ZAIDI: Toka ilipoingia madarakani serikali ya awamu ya tano imejipambanua vyema isivyokuwa muumini wa demokrasia, Katiba na hata sheria za nchi yetu. Imekuwa ni serikali inayoongozwa kwa matamko na kauli kana kwamba ni nchi iliyotoka vitani. Itakumbukwa tamko la kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara lililotolewa na Rais John Pombe Joseph Magufuli wakati anawahutubia wanachama wa CCM mkoani Singida mwaka 2016. Tamko hilo pamoja na kuwa kinyume cha Katiba na sheria za nchi linaendelea kushikiwa bango na vyombo vya ulinzi na usalama kuwabana wapinzani wakati chama tawala (CCM) kinaendelea na shughuli zake za kisiasa mahali popote bila pingamizi lolote. Wakati tunaendelea na jitihada za kuipinga amri hiyo haramu, tayari serikali imepeleka Bungeni Muswada wa sheria ya vyama vya siasa unaokusudia kuihalalisha na kufanya shughuli za kisiasa kuwa suala la jinai. Aidha Muswada huo unalenga kumfanya Msajili wa vyama vya siasa kuwa mamlaka ya usimamizi (Regulatory Authority) na hivyo kuwa na uwezo wa kuingilia shughuli za kiutawala (Administrative Affaires) na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa; hususan, kusimamisha na kufukuza wanachama. Ni Muswada unaolenga kupata sheria kandamizi kwa minajili ya kufifisha ushindani wa kweli wa kisiasa unaotokana na nguvu tofauti kwa sababu ya vyama vya siasa kujijengea uwezo wa kupambana kwa hoja (capacity to stand up on the opinion of the other). Lengo ni kuisaidia CCM iliyochoka na kufilisika kuendelea kutawala kwa msaada wa dola na taasisi zake. Katika tamko la viongozi waandamizi wa vyama vya siasa waliokutana Mtoni, Zanzibar tarehe 16 18 Desemba, 2018, kuitafakari hali ya mdororo wa demokrasia nchini (democratic recession) ili kuona namna ya kulinasua Taifa letu kutoka hali hiyo na kurudi kwenye njia itakayotupeleka kwenye Ujenzi wa Demokrasia Madhubuti, ilibainishwa kuwa njia mojawapo ni kupitia Mahakama kwa kufungua kesi za kimkakati (strategic litigations). Leo tumewaita wanahabari; na kupitia kwenu Watanzania wote, kuwajulisha kuwa tayari utekelezaji wa maazimio yanayotokana na tamko hilo umeanza. Tayari vyama kumi vya upinzani vimefungua shauri Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es salaam, kupinga Muswada wa sheria ya vyama vya siasa kujadiliwa na Bunge kwa minajili ya kuupitisha kuwa sheria. Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura (Certificate of Urgency) tarehe 20/12/2018 na kusajiliwa kwa Na.30 la 2018. Walalamikaji (Applicants) kwa niaba ya vyama ni Waheshimiwa Joran Lwehabura Bashange, Salim Abdalla Rashid Bimani na Zitto Zuberi Kabwe. Mlalamikiwa (Respondent) ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tayari wasomi mawakili wetu Mpare Kaba Mpoki na Daimu Halfani wakwekwisha jiandaa kuwasilisha hoja zetu mara mahakama itakapopanga majaji kwa ajili hiyo. Na kama zilivyofanya Mahakama za nchi za Kenya na Malawi kukhairisha likizo ya majaji ili kushughulikia mashauri ya kikatiba kama haya tunatoa wito kwa Mahakama Kuu kulichukulia uzito shauri letu. Shauri hilo ni la kikatiba na msingi wake unatokana na mapendekezo ya Tume ya jaji Francis Lucas Nyalali (Nyalali Commission on multiparty Democracy) ambayo ilipendekeza aidha marekebisho au kufutwa sheria 40 ambazo zilionekana kandamizi, zinakiuka Katiba na kupitwa na wakati kwa vigezo vifuatavyo; Kunyanganya uhuru wa wananchi (freedom) Kunyanganya haki za msingi (basic rights) Kubinya uhuru wa haki za msingi (impingement of freedom) Muswada wa sheria ya vyama vya siasa ukisomwa na kuchambuliwa kwa ujumla wake, iwapo utajadiliwa na kupitishwa kuwa sheria; jambo ambalo linawezekana sana kutokana na wingi wa wabunge wa CCM ambao itikadi kwao ni zaidi ya maslahi mapana ya taifa, ni dhahiri sheria hiyo itanyanganya uhuru (freedom), haki za msingi (basic rights) na kubinya uhuru wa haki za msingi (impingement of freedom) mambo ambayo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) katika ibara za 18, 20 na 21. Uwezo wa kufungua shauri hilo unatokana na katiba yenyewe na sheria ya Haki na wajibu wa Msingi (Basic Rights and Duties Enforcement Act Cap 3 of 1995) ambazo kwa pamoja zinatoa uwezo kwa mtu yoyote kufungua shauri Mahakama Kuu kama anahisi kuwa masuala yanayohusiana na haki na wajibu wake kwenye katiba katika ibara za 12 mpaka 29; zimevunjwa, zinavunjwa au zinaelekea kuvunjwa. Mahakama Kuu inao uwezo wa kusikiliza na kufanya uamuzi juu ya shauri lolote la jinsi hiyo lililoletwa mbele yake. Tumefanya hivyo kutimiza wajibu wetu wa kikatiba kuhakikisha kuwa hatumuonei haya yeyote anayevunja au kufanya vitendo vya kuvunja katiba ya nchi yetu. Aidha tumeamua kuunganisha nguvu kufanya kwa pamoja kwa sababu kwa sasa; ni lazima kukubali ukweli kuwa, kwa hali ya nchi ilivyo sasa hakuna chama kimoja pekee ama asasi za kiraia au kundi la jamii moja pekee linaweza kukabili utawala dhalimu wa kidikteta uliopo nchini na kushinda. Tunatoa wito kwa Watanzania wote, wanahabari, wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wanaharakati, asasi za kiraia, viongozi wa taasisi za kiraia na kidini, na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla, kuungana nasi na kwa pamoja kushikamana katika vita hii na hatupaswi kuruhusu kuendelea na hila za utawala huu wa kidhalimu kwani ni hatari kwa demokrasia yetu, hatari kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu na uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja. Hili ni jambo linalowezekana iwapo tutakuwa na mshikamano madhubuti bila kujali vyama vyetu vya siasa, asasi za kiraia au makundi ya kijamii tunayotoka. Inawezekana tutimize wajibu wetu. USHIRIKIANO IMARA NA MADHUBUTI (THE GRAND COALITION) Joran Lwehabura Bashange, Naibu Katibu Mkuu Bara (CUF) Salim Abdalla Rashid Bimani, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma (CUF) Zitto Zuberi Kabwe, Kiongozi wa Chama, (ACT-Wazalendo)