PICHA:MICHUANO YA COPA -UMISSETA YAZINDULIWA KWA KISHINDO DODOMA



Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jaffo
akisalimiana na baadhi ya wachezaji wa timu zilizoshiriki uzinduzi wa
michezo ya shule za sekondari nchini (Copa-UMISSETA) katika uwanja wa
Jamhuri mjini Dodoma jana, mara baara ya uzinduzi rasmi wa michuano hiyo
itakayoendeshwa nchini kote kwa udhamini wa kampuni ya vinywaji baridi
ya Coca-Cola. Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na wanafunzizaidi ya elfu
20 kutoka shule mbalimbali za sekondari mkoani Dodoma. (Picha na Mpiga
Picha Wetu, Dodoma).
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jaffo akipiga
penati kuashiria uzinduzi wa michezo ya shule za sekondari nchini
(Copa-UMISSETA) katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana, mara baara
ya uzinduzi rasmi wa michuano hiyo itakayoendeshwa nchini kote kwa
udhamini wa kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola. Hafla ya uzinduzi
ilihudhuriwa na wanafunzizaidi ya elfu 20 kutoka shule mbalimbali za
sekondari mkoani Dodoma. (Picha na Mpiga Picha Wetu, Dodoma).
Vifaa vya michezo.

* Wanafunzi zaidi ya elfu 20 kutoka sekondari wahudhuria
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Kiu ya wanafunzi na wadau wa michezi nchini kote kuhusiana na mashindano
ya michezo na sanaa kwa shule za sekondari nchini imekatwa rasmi siku
ya jana, baada ya kufanyika uzinduzi wa michuano hiyo kwenye uwanja wa
Jamhuri, Dodoma.
Akifungua michuano hiyo kwa mkoa wa Dodoma,Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jaffo alitoa pongezi kwa mchango wa kampuni
ya Coca-Cola kuendeleza michezo mashuleni, huku akiwataka wakurugenzi
wa halmashauri kote nchini kuhakikisha kuwa wanatenga viwanja vya
michezo.
Vile vile, aliwaelekeza maafisa elimu ngazi ya tarafa, kata, wilaya,
mikoa pamoja na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha kuwa
vipindi vya michezo mashuleni vinaimarishwa na kutumika kwa ajili ya
shughuli za michezo na si kufundisha masomo mengine.

“Mtoto anayekosa kushiriki michezo, hata akili yake huweza kufubaa.
Michezo hujenga na kuimarisha afyaya mwili na akili, upendo, ushirikiano
na uzalendo”, alisema Jaffo.
Aidha, aliongeza kuwa wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na
makaibu tawala wa mikoa kuhakikisha kuwa kila shule ina viwanja vya
michezo vyenye vipimo sahihi na kusimamia sharia ya elimu inayotaka
shule inaposajiliwa lazima kuwa na eneo la viwanja vya michezo.
Ofisi ya Rais Tamisemi haitowaangusha walimu wote wa michezo nchini katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, wakati akihutubia hafla ya ufunguzi wa michuano hii,
mwakilishi wa kampuni ya Coca-Cola nchini, Pamela Lugenge
aliwahakikishia washiriki kuwakampuni hiyo itaendelea na dhamira yake ya
kuunga mkono jitihada ya vijana mbalimbali nchini kote katika
kuwasaidia kudhihirisha vipaji vyao kupitia mashindano mbalimbali ya
michezo, ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa udhamini wa michuano ya
Copa-UMISSETA.


“Dhamira yetu katika kudhamini mashindano haya na kushirikiana TAMISEMI
ni endelevu, tukiwa tumejidhatiti kuhakikisha tunaendelea kuunga mkono
jitihada za kutambua na kuinua vipaji vya vijana ambao watakuja
kuifikisha nyanja ya michezo nchini katika kiwango cha juu zaidi”,
alisema Pamela.
Mbali na hayo, aliongeza kuwa “Pamoja na kuwepo changamoto ndogondogo
za hapa na pale, tutaendelea kufanya kazi bega kwa bega na washirika
wetu serikalini, pamoja na wadau wengine wote wa michezo nchini, ili
kwa pamoja tuweze kufanikisha na kusaidia kukua kwa sekta ya michezo
nchini, hususani mashindano ya mpira wa miguu pamoja na mpira wa kikapu
kwa vijana”.
Alimalizia kwa kuwahakikishia wadau wa michezo nchini ya kwamba kwa
mwaka huu kampuni ya Coca-Cola imejipanga kwa dhati, kudhihirisha ya
kwamba michezo ni zaidi ya ushindani, kwa kuweza kuambatanisha
mashindano haya na kujenga mshikamano wa timu shindani, urafiki na hata
nidhamu kwa wachezaji na timu zinazoshiriki.


