Kenya
na Ushelisheli zimesaini makubaliano ambayo yataimarisha nchi hizo
mbili na kupanua ushirikiano baina yao katika biashara na usalama.
Makubalioano hayo yalifikiwa wakati Rais Uhuru Kenyatta alipofanya
mazungumzo na mgeni wake Rais Danny Faure wa Ushelisheli katika ikulu ya
Nairobi jana.
Rais wa Ushelisheli Danny Faure jana asubuhi aliwasili nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku tatu.
Mkutano baina ya viongozi hao wawili ambao ulifanyika katika
ikulu ya Nairobi,uliafikia makubaliano ambayo yatafanikisha kwa wakenya
waliohitimu kutafuta ajira nchini Ushelisheli kwa sababu taifa hilo
linahitaji mtaji wa rasilimali watu walio na taaluma kwa ajili ya uajiri
katika sekta mbalimbali za uchumi wake.
Aidha taifa la Kenya litaweza kuuza bidhaa nyingi za kilimo nchini Ushelisheli.
"Tumezungumza kuhusu jinsi gani Ushelisheli inaweza kuisaidia
Kenya katika kuinua uchumi wetu wa samawati na usalama wa
baharini.Tumejadiliana na kukubaliana kuhusu vipi tunaweza kuimarisha
ushirikiano wetu kuhusu Kenya kusafirisha maua na bidhaa za kilimo
Ushelisheli,nyama,kuku na bidhaa za maziwa"
Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wao
jana,Rais Kenyatta na Rais Faure walitangaza kuwa Ushelisheli itaisaidia
Kenya kuifanya bandari ya Mombasa kuwa na uwezo wa kuwa bandari ya
usafirishaji wa samaki.
Rais Faure alisema Ushelisheli iko tayari kufanya kazi na Kenya na kuisaidia kupanua sekta ya uvuvi.
"Ushelisheli iko tayari kufanya kazi na wewe Rais Kenyatta na
serikali yako kuweka mfumo mpya ambao tutawasaidia kukuza sekta yenu ya
uvuvi na sekta ulinzi.Tumekubaliana kwamba kufikia mwezi Juni hadi Julai
tuwe na tume ya pamoja baina ya nchi hizi mbili ambayo itaweka makataa
ya kufikiwa kwa hatua hizi"
Aidha alisema ushirikiano baina ya nchi hizi mbili unaweza
kuimarishwa kupitia mipango mengine kama vile ubadilishanaji wa taarifa
za ujasusi na mipango ya kujenga uwezo.
Rais Faure alisema utalii ni kitega uchumi kikuu cha fedha za
kigeni kwa Kenya na Ushelisheli,na nchi hizo mbili zote zina bidhaa
sawa-utalii wa fukwe za bahari.
Aidha alisema ni vyema kwa nchi hizo kushirikiana ,na nchi zote
mbili zitanufaika kwa sababu kuna fursa nyingi za ushirikiano katika
sekta hiyo.
"Sasa tutaangalia ukuzaji wa vituo viwili vya utalii.Nyinyi mna
utalii wa safari katika mbuga za wanyama na sisi tuna utalii wa fukwe za
bahari,kwa hivyo tumekubaliana kwamba mashirika yetu yote ya mauzo na
mawaziri watashirikiana katika kubadilisha maono haya kuwa kweli"
Fursa hizo zitajumuisha ugawanaji wa njia
bora,mafunzo,ubadilishanaji wa mipango ,mikakati ya pamoja ya mauzo na
ufungaji wa pamoja wa sehemu za kuzuru.
"
Rais Kenyatta alisema pia wamezungumza kuhusu uwezo wa Kenya wa kusafirisha walimu kufunza nchini Ushelisheli.
Aidha Rais Kenyatta alitoa shukrani kwa Rais Faure na serikali
yake kwa kuimarisha usalama dhidi ya maharamia na katika kupambana na
vita dhidi ya dawa za kulevya.
"Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais Faure kwa ushirikiano
na umoja ambao maafisa wetu wa usalama wamepata katika vita dhidi ya
uharamia ,ugaidi,na hasa katika vita dhidi ya madawa ya kelvya.Ni kweli
kwamba ushirikiano ambao tumepata kutoka taifa la Ushelisheli
tumefanikiwa kupata ushindi ambao tumeupata katika siku za nyuma
.Nachukua fursa hii kumshukuru Rais Faure na serikali kwa msaada huo"
Ziara hii ya Rais Danny Faure wa Ushelisheli nchini Kenya ni ya
kihistoria.Kenya ni nchi ya kwanza ambayo Rais Faure amezuru tangu awe
rais miezi sita iliyopita.
KENYA NA USHELISHELI ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA NA USALAMA.
Reviewed by Unknown
on
8:31 AM
Rating: 5