PADRI WA KANISA KATOLIKI ATIWA MBARONI KISA KIROBA.
Polisi mkoani Ruvuma inamshikilia Padri
wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kitanda wilayani Namtumbo, Gislary Tweve
kwa tuhuma za kumshambulia mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kitanda, Adolf
Nyoni (34) baada ya kukataa kulipa kinywaji aina ya Konyagi,
kilichokuwa katika kifungashio cha plastiki (kiroba) alichokunywa katika
duka la kanisa hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zuberi Mwombeji alisema padri huyo anadaiwa
kutenda kosa hilo Machi 10, mwaka huu, saa mbili usiku katika duka la
Parokia ya Kitanda.
Kamanda Mwombeji alisema Padri Tweve alimpiga Nyoni kichwa na makofi,
kisha kumrukisha kichura kwa kile kinachodaiwa kukataa kulipa pombe hiyo
ambayo imekatazwa kisheria, lakini duka hilo bado limekaidi na
kuendelea kuuza pombe hiyo.
Alisema Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na mara utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma,
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali katika vyombo vya
dola, badala ya kuichukulia sheria mkononi na kuachana na biashara
iliyopigwa marufuku ya pombe kali zilizofungwa kwenye vifungashio vya
plastiki.
Kuanzia Machi mosi, mwaka huu, serikali imepiga marufuku utengenezaji,
usambazaji, uuzaji na unywaji wa pombe zilizowekwa katika vifungashio
vya plastiki maarufu kwa jina la viroba, na kuibainisha kuwa itatoa
adhabu zikiwemo faini za hadi Sh milioni tano, kifungo jela au vyote kwa
pamoja, kwa watakaokiuka marufuku hiyo.
Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kubainika kwamba mbali ya
kuikosesha mapato serikali yanayofikia Sh bilioni 600 kwa mwaka, pombe
hizo za kwenye viroba zimekuwa zikitumiwa isivyo kutokana na ufungashaji
wake wa kirahisi.
Aidha, katika matukio mengine, Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wakiwa katika operesheni ya dawa za
kulevya na pombe za viroba, wamemkamata mfanyabiashara Lucy Mbilinyi
akiwa na pombe za viroba aina mbalimbali katoni 50 zenye thamani ya Sh
5,454,000.
Kamanda alisema Mbilinyi alikamatwa saa 10 jioni maeneo ya Tunduru mjini akiwa anaendelea kuuza pombe hiyo kinyume cha sheria.
Pia polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TFDA, wamemkamata mkazi wa
Majengo katika Manispaa ya Songea, Bruno Boniventura (50) akiwa na pombe
za viroba aina ya Zanzi, Officers katoni nane na boksi 11 zenye thamani
ya Sh 1,040,000.
Katika hatua nyingine, Polisi mkoani Ruvuma imewatia mbaroni watu
wawili, Athumani Likungwa na Ridhiwani Msaka ambao ni wakazi wa Ulambani
Ligera wakiwa na bunduki aina ya gobori waliyokuwa wakimiliki kinyume
cha sheria.
Kamanda Mwombeji alisema watu hao walikamatwa Machi 13, mwaka huu saa
nane mchana katika Kijiji cha Undendeule, Kata ya Undendeule Tarafa ya
Songea Mashariki wilayani Songea wakiwa na silaha hiyo.


