Hatimaye Wizara Zimehamia Dodoma Asilimia 100.

Azma ya serikali ya kuhamia Dodoma imetimia kwa asilimia 100 kutokana na
wizara takribani zote kuhamia mjini Dodoma. Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi John Kijazi ametoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati
akizungumza na Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu ambao kwa mara ya kwanza
wamefanya vikao vyao mjini hapa tangu serikali ilipofanya uamuzi wa
kuhamia hapa.
“Mkutano wa Kamati Maalumu wa Makatibu Wakuu wa wizara zote ni kielelezo
dhahiri cha utekelezaji wa azma ya serikali kuhamia Dodoma,” ameeleza.
Balozi Kijazi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, alisema hadi
kufikia Machi mosi mwaka huu, takribani wizara zote zimehamia Dodoma,
utaratibu huo ambao ulizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Septemba 30, 2016.
Amewashukuru Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na
Serikali ya Awamu ya Tano, lakini pia alitoa rai kwa wananchi kuzitumia
fursa zilizopo mjini hapa za biashara na uwekezaji, huduma mbalimbali za
kiuchumi na kijamii pamoja na kujenga Tanzania mpya.
Kuhamia mjini hapa, kunaifanya awamu ya kwanza ya mpango wa Serikali wa
kuhamia kwa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu na
baadhi ya wakurugenzi uwe umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na sasa macho
yanaelekezwa katika awamu ya pili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema tayari ofisi yake
inapokea taarifa za idadi ya watendaji waliohamia Dodoma.
“Tayari ninapokea taarifa za mawaziri, makatibu na watendaji wa wizara
kuhamia Dodoma na naziweka sawa, nitakaa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
ili kuziweka hadharani,” amesema Jenista, na kuongeza kuwa baada ya
kuzihakiki na Waziri Mkuu, ndipo atazungumza na vyombo vya habari kuhusu
kuhamia Dodoma.
Amesema kazi ya kukusanya taarifa ikikamilika, serikali itatoa taarifa
kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la
kukamilika kwa awamu ya kwanza Februari 28, mwaka huu, namna
lilivyokwenda.
Katika kuhama huko kwa serikali, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimetoa
mchango mkubwa wa kuruhusu wizara nane kutumia majengo yake pamoja na
Mfuko wa Serikali za Mitaa (LAPF) wizara tatu, na Hazina Ndogo
iliyopokea wizara mbili


