KAHAMA WAIPONGEZA SERIKALI KUHUSU VIROBA....WATAKA UGORO NAO UZUIWE.
Kutokana na serikali kupiga marufuku kuuzwa kwa pombe zenye vifungashio
vya plastiki (viroba) kuanzia jana, baadhi ya wananchi mjini Kahama
wameipongeza hatua hiyo na kuiomba pia ihamishie nguvu pia katika kupiga
marufuku ugoro ambao umekuwa ukitumiwa na vijana wengi wilayani Kahama
mkoani Shinyanga.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, baadhi ya vijana mjini
Kahama wameipongeza serikali kupiga marufuku pombe hiyo huku baadhi yao
wakishauri kuwa nguvu kubwa sasa ielekee katika kupiga marufuku matumizi
ya ugoro ambayo ni makubwa na yanaweza kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Walisema aina hiyo ya kilevi ya ugoro ambayo ilikuwa ikitumiwa na vijana
katika kiwango cha chini katika siku za nyuma, lakini kwa sasa matumizi
yake yamekuwa makubwa kutokana na mapambano dhidi ya dawa za kulevya
yanayofanywa na serikali.
“Tunaomba serikali iangalie kwa upande wa pili ambao ni matumizi ya
ugoro ambao kwa sasa imekuwa ni tatizo kubwa kwa vijana baada ya
kupambanza moto kwa dawa za kulevya kunakofanywa na Serikali. Kwa sasa
dawa hizo hazipatikani kwa urahisi,” alisema mmoja wa wakazi wa Kahama,
Selestine Bitende.
Alisema biashara ya ugoro ambayo imeibuka katika maeneo mbalimbali
nchini, imekuwa ikiwapatia kipato kikubwa wauzaji kutokana na watumiaji
wake kuwa wengi kwa sasa hali ambao kwa siku za baadaye inaweza ikaleta
matatizo makubwa kwa vijana kama ilivyo kwa dawa za kulevya.
Bitende aliongeza kuwa wanaiomba serikali kupitia vyombo vya habari
kuhakikisha kwa matumizi haya ya ugoro kwa vijana yanatokomezwa kama
ilivyo kwa vita vingine ili kujenga Taifa la Vijana ambao wanaweza
kulitumia Taifa katika siku za baadaye.
Edward Charles alisema suala la vijana kuvuta ugoro kwa sasa linafaa
kukemewa kwa hali ya juu kwani hali ni mbaya kwa baada ya serikali
kupambana na dawa za kulevya vijana hao wamehamia katika utumiaji wa
ugoro.
“Unakuta mtu amebandika kibao katika mti kuwa ugoro mkali unapatikana
hapa, ni lazima kutakuwa na mchanganyiko aidha wa madawa ya kulevya au
vitu vingine kwani kwa uhalisia kilevi aina ya ugoro, pia kina ukali
kama ilivyo kwa madawa ya kulevya mengine,” alieleza Charles.
Hivi karibuni, serikali ilitangaza vita dhidi ya dawa ya kulevya pamoja
na wauzaji wake huku baadhi ya vijana waliokuwa wakitumia dawa
wakionekana kuathirika kutokana na kutopatikana kwa urahisi kwa sasa
hali iliyowafanya kuhamia katika kilevi kingine aina ya ugoro ambacho
kinapatikana kwa urahisi tofauti na ilivyo kwa dawa za kulevya.


