Mgogoro baina ya Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia na mkuu wa
wilaya hiyo, Saimon Odunga umechukua sura mpya, safari hii ukiibuka
katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dodoma (RCC) ambayo
imeamua ufikishwe kwa Waziri Mkuu.
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana kilifanyika
katika ukumbi wa Chuo cha Mipango.
Baada ya Odunga kupewa nafasi ya kuchangia ajenda mara baada ya Majaliwa
kuondoka, aliomba ushirikiano kutoka kwa wabunge ilikutekeleza shughuli
za maendeleo.
“Ninaomba waheshimiwa wabunge watusaidie kulisemea hili kwa sababu hali ni mbaya katika sekta nyingi,” alisema.
Akizungumza katika kikao hicho, Nkamia, ambaye aliwahi kuwa naibu
waziri, alianza kwa kumuomba Rugimbana kusaidia katika sekta ya ardhi
akisema ina matatizo mengi na kutoa mfano wa Wilaya ya Chemba.
Alisema katika wilaya hiyo kuna tapeli wa ardhi ambaye amesaidiwa na
viongozi kupata ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 kinyume na sheria.
Alihoji sababu za mkuu huyo wa wilaya kutaka wabunge washiriki katika
kusukuma hoja mbalimbali za maendeleo, wakati anadharau wabunge,
mwenyekiti wa halmashauri na viongozi wengine wa chama wilayani humo.
“Huyu ni mkuu wa wilaya ambaye anaongoza kwa rekodi ya kuwakamata watu
kwa kutumia madaraka yake. Nimesikia jana (juzi) kuwa na mimi nawindwa
ili nikamatwe. Niko tayari kukamatwa,” alisema Nkamia, ambaye anaongoza
Jimbo la Chemba kwa kipindi cha pili mfululizo.
“Nakuomba mkuu wa mkoa umuite huyu dogo (DC) umkanye kuhusu hii tabia
yake ya kudhalilisha watu. Kwa kuwa bwana mkubwa (DC) hapo ameanzisha
vita na sisi tunaomsaidia kazi. Sisi tuna busara zetu, hatuwezi kuingia
vitani,” alisema.
Nkamia alimuomba Rugimbana kuwaita wote wawili-Odunga na yeye-wakae
pamoja na kutafutia suluhu ya jambo hilo ambalo alisema linaweza
kukwamisha maendeleo ya jimbo hilo.
Alimuonya mkuu huyo wa wilaya kuhusu tabia ya kuwatia mbaroni wananchi wanaouliza maswali wakati ni haki yao kufanya hivyo.
“Chemba tulikuwa tunaishi kwa amani sana lakini amekuja bwana huyu mdogo
(Odunga) anataka kutuchafulia sifa sisi. Ameteuliwa na Rais amefanyiwa
vetting (uhakiki) nzuri tu. Mambo ya kuwaita watu wapumbavu no
(hapana),” alisema Nkamia.
Waziri Mkuu apokea ugomvi wa DC na Mkuu wa wilaya
Reviewed by Mipiko
on
8:07 PM
Rating: 5