Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema haitaongeza siku
za kufanya uhakiki wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) hapa
jijini baada ya muda kumalizika leo, hivyo wote watakaokuwa
hawajahakikiwa watafutiwa namba zao na watatakiwa kuomba upya.
Kwa mara ya kwanza TRA imepanga kufanya uhakiki wa TIN kwa siku 60 kati
ya Agosti na Oktoba lakini baada ya kujitokeza watu wengi tarehe ya
mwisho iliongezwa hadi Novemba na mara ya tatu ilisogezwa hadi Januari
31. Lengo la uhakiki huo ni kuondokana na mfumo wa kizamani wa usajili
wa namba hiyo.
Kayombo alisema kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wanahitaji
kuhakikiwa namba, mamlaka iliamua kusogeza mbele muda wa kutoa huduma
hiyo pamoja na kufungua vituo vya kutoa huduma ambako watumishi
walifanya kazi hiyo hadi Jumamosi na Jumapili kuwapa nafasi wafanyakazi.
Alisema madhara kwa watakaofutiwa TIN ni makubwa kwani wafanyabiashara
na madereva wa magari leseni zao zitakuwa batili na watachukuliwa hatua
kwa kosa la kufanya biashara bila kuwa na namba ya utambulisho.
“Wale wote ambao watakuwa hawajahakikiwa watafutiwa namba zao za TIN,
itawalazimu kuomba upya ingawa kuomba kwao upya hakutafuta madeni yao ya
nyuma,” alisisitiza Kayombo.
Mmoja wa watu waliokwenda kuhakiki namba zao kituo cha Mwenge, Abdul
Namwelesi alikosoa utaratibu huo akipendekeza uhakiki ungekuwa endelevu
badala ya kuweka muda maalumu kutokana na ugumu wa watu wote kuhakikiwa
kwa wakati mmoja.
Alisema kutokana na ratiba ya maisha hususani kwa wakazi wa Dar kuwa za
kukimbizana, TRA wangeweka utaratibu maalumu kila dereva anapokwenda
kuhuisha leseni yake ahakikiwe taarifa zake na kila mfanyabiashara
anapokwenda kulipa kodi hapohapo ahakikiwe taarifa zake.
Zulekha Kambi aliyekutwa kwenye kituo cha Uwanja wa Taifa alijilaumu
kutokana na kutotumia muda mrefu uliokuwa umetolewa badala yake
akasubiri hadi siku za mwisho zenye msongamano mkubwa.
“Najuta. Wee acha tu. Nilikuwa likizo nyumbani mwezi mzima. Jana ndiyo
nimekumbuka kesho mwisho. Nimekuja na nimekuta umati kama huu. Hapa
nilipo hata fomu sijui nitaipata saa ngapi,” alisikitika.
Usajili wa TIN Dar wafikia kikomo
Reviewed by Mipiko
on
8:16 PM
Rating: 5