Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea
utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro
kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo
mchana na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema
taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
“Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo
tukimaliza sherehe za maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana
kuhusu taarifa yenu,” amesema.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema
hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto
26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26
sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili
kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili Robert
Mande (Kushoto) na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Bw.
Nollasco Ngowe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016
afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka
huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na
Faru. Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu
wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert
Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa
kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu
aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee
nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’
kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.
Taarifa ya kifo cha faru John yakabidhiwa kwa Waziri Mkuu
Reviewed by Mipiko
on
6:33 PM
Rating: 5