Michael Flynn Jnr (kushoto) na babake, Luteni Jenerali Mstaafu Michael Flynn Snr wakiwaTrump Tower in New York
Mmoja wa wasaidizi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump amepoteza
kazi kwa kuendeleza uvumi ambao ulifikia kilele chake katika ufyatuaji
wa risasi katika mgahawa mmoja wa pizza wikendi.
Michael Flynn, 33, aliacha kazi katika kundi la mpito la Bw Trump
Jumanne kwa sababu ya ujumbe alioandika kwenye Twitter kuhusu habari za
uongo.
Sakata hiyo sasa inafahamika kama Pizzagate.
Babake, Michael Flynn Snr, ambaye ameteuliwa na Bw Trump kuwa mshauri mkuu wa usalama wa taifa, pia alisambaza habari za uongo.
Uvumi huo wa Pizzagate ulisababisha mtu mwenye bunduki kufyatua risasi mgahawani Jumapili.
Hakuna aliyejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea katika mgahawa wa Comet Ping Pong mjini Washington DC.
Mshukiwa huyo aliwaambia polisi kwamba alikuwa amefika eneo hilo
"kuchunguza mwenyewe" uvumi ulioenezwa mtandaoni kwamba mgahawa huo
ulikuwa ngome ya kundi la watu wanaowadhulumu watoto ambalo lilihusisha
Hillary Clinton na mmoja wa wasaidizi wake, John Podesta.

Edgar Maddison Welch, 28, akijisalimisha kwa polisi Jumapili
Uvumi huo ulikuwa umeenezwa na blogu za makundi yanayoegemea siasa za mrengo wa kulia.
Madai hayo pia yalienezwa na Bw Flynn Jr, ambaye Jumapili, baada ya
ufyatuaji wa risasi kutokea katika mgahawa huo, alisema habari hizo
zitasalia kuwa za kweli "hadi zithibitishwe kuwa za uongo."
Gazeti la New York Times linasema alifutwa kutoka kwenye kundi la mpito
la Bw Trump Jumanne, lakini kwa mujibu wa CBS News, alijiuzulu kabla ya
kufutwa.
Maafisa wa Trump wamethibitisha kuondoka kwa Bw Flynn, ambaye tayari
alikuwa amepewa anwani ya barua pepe ya serikali inayoisha na .gov,
lakini hawakusema iwapo kuondoka kwake kunahusiana na ujumbe wake katika
Twitter.

Makamu wa rais mteule Mike Pence amekiri kwamba Bw Flynn Jnr alikuwa
anamsaidia babake katika masuala ya ratiba na kiutawala kipindi hiki cha
mpito lakini sasa hana tena majukumu hayo.
Babake, Bw Flynn Snr, 57, pia amewahi kusambaza kwenye Twitter uvumi wa
kudai Bi Clinton na wasaidizi wake, walihusika katika ulanguzi wa
watoto.
Luteni jenerali huyo mstaafu pia amewahi kudai kwamba Rais Barack Obama
ni "mwanajihadi" ambaye "analangua na kutakasa" pesa kwa niaba ya
magaidi.
Katika kisa cha Jumapili, mshukiwa Edgar Maddison Welch, 28, anayetoka
North Carolina, aliingia Comet Ping Pong na kumwelekezea mfanyakazi
mmoja bunduki lakini baadaye akafyatua risasi sakafuni.
Ameshtakiwa kwa kumshambulia mtu akitumia silaha hatari.
Kashfa ya Pizzagate ilianzaje?
Uvumi wa Pizzagate ulianza kwenye mtandao wa 4chan, kwa kutumia habari
kuhusu barua pepe za chama cha Democratic ambazo zilikuwa zimefichuliwa
na Wikileaks.
Mmiliki wa mgahawa huo, James Alefantis, ambaye ni mfadhili wa
Democratic, alitajwa kwenye barua pepe hizo kuhusiana na hafla ya
kuchangisha pesa za kampeni za Democratic.
Watu wanaotumia 4chan na mtandao mwingine wa Reddit, walianza kudai
maneno kama vile jibini, hot dog na pizza yalikuwa maneno ya siri ya
kuwarejelea watoto na ngono.