Umoja wa Mataifa kuimarisha kikosi chake cha kusimamia amani CAR

Mkurugenzi wa Masuala ya Mawasiliano ya Wasimamia Amani wa Umoja wa
Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametangaza kuwa, umoja huo una
mpango wa kuimarisha zaidi kikosi chake katika nchi hiyo.
Hervé Verhoosel ameeleza kuwa, Umoja wa Mataifa umeazimia kuongeza idadi
ya askari wake wa kusimamia amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Verhoosel ameelezea kuwa, shughuli ya kusimamia amani ya kikosi hicho
kinachojulikana kama MINUSCA zitapanuka katika maeneo mengine ya nchi
hiyo.
Umoja wa Mataifa unatangaza uamuzi wake wa kupanua shughuli za kikosi
chake cha kusimamia amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati katika hali
ambayo, huko nyuma askari wake wamewahi kukabiliwa na tuhuma nyingi za
vitendo vya kubaka na kunajisi.

Kikosi cha kulinda amani chah UN nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA)
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko na mapigano tangu
mwaka 2013 wakati makundi ya Kikristo yanayobeba silaha yalipoanzisha
mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi
zaidi, ambalo mnamo mwezi Machi mwaka huo liliiondoa madarakani
serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Francois Bozize.
Kufuatia machafuko hayo raia wengi wameyakimbia makazi yao na kuishi
maisha ya ukimbizi ndani na nje ya nchi hiyo. Takwimu za Umoja wa
Mataifa zinaonyesha kuwa, karibu raia laki nne wa Jamhuri ya Afrika ya
Kati wamekuwa wakimbizi huku kumi na moja elfu kati yao wakiomba hifadhi
katika nchi jirani.


