Kibao chabadilika...Sasa "Neema" kuwashukia walimu waliomchapa Mwanafuzi Mbeya Day.Soma maamuzi yao mapya hapa

Baada ya uamuzi wa kuwafukuza vyuo walimu wanne waliokuwa kwenye
mafunzo ya vitendo katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya (Mbeya
Day), serikali imesema vyuo husika vinaweza kushauri adhabu mbadala
iwapo vitajiridhisha kuwepo kwa mazingira tofauti na yaliyozingatiwa
kwenye uamuzi wa kuwafukuza vyuo.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari
mkoani Mbeya alikokuwa katika ziara kwenye shule mbalimbali mkoani humo.
Profesa Ndalichako alisema uamuzi uliochukuliwa na ofisi yake
ulizingatia sheria ndogo zilizotungwa katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (Udsm) zinazoainisha makosa yanayoweza kumfukuzisha chuo
mwanafunzi.
Hata hivyo, alisema uamuzi uliochukuliwa unaweza kutazamwa upya na vyuo
husika iwapo uzito uliochukuliwa na wizara utaonekana kuwa katika
mazingira na uhalisia wa tukio husika.
Walimu wanne waliokuwa kwa vitendo katika shule ya Mbeya Day walifukuzwa
vyuo baada ya uamuzi wa serikali kutokana na kuhusika kumpiga
mwanafunzi Sebastain Chinguku vibao, mateke na fimbo kwa ukatili
Septemba 28 mwaka huu shuleni humo.
Walimu hao walibainika baada ya kipande cha video kusambazwa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni.
Waliohusika na vyuo walivyokuwa wakisoma ni Frank Msigwa (anayedaiwa
kumpiga zaidi mwanafunzi makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka
wote wa DUCE-UDSM, na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere.
Akijibu swali la idadi ipi ya viboko inastahili kutolewa kama adhabu kwa
mwanafunzi anayekwenda kinyume na maelekezo ya shule yake, Profesa
Ndalichako alisema binafsi asingependa mwanafunzi achapwe hata kiboko
kimoja lakini hilo linawezekana pale wanafunzi watakapozingatia maadili.
“Adhabu yoyote kwa mwanafunzi inatolewa pale anapokuwa amekwenda kinyume
na maadili ya shule yake. Kama wanafunzi wote watazingatia maadili
sidhani kama kuna mwalimu atakayempiga mwanafunzi hata kiboko kimoja.
Haya yote yanatokea kutokana na wanafunzi kukosa nidhamu,” alisisitiza
Ndalichako.
Aliwasihi wanafunzi kuzingatia maadili ya shule yao, akisema ndiyo njia
pekee ya kuwawezesha kuishi vyema na walimu wao na pia kufanya vyema
kitaaluma na kuwasihi wazazi kuwafundisha watoto wao nidhamu ya
kuwaheshimu watu wote, akisema malezi hayo yatawapunguzia walimu adha ya
kuishi na wanafunzi watukutu ambao kimsingi wanazorotesha utendaji kazi
wao.


