ASKARI POLISI APATWA KIGUGUMIZI KUSIMAMIA SHERIA
Askari Polisi wa Kampuni ya Reli
Tanzania (TRL), akipiga picha gari lenye namba T 297 AQE baada ya dereva
wa gari hilo kukiuka sheria ya usalama barabarani kwa kusimama kwenye
reli katika makutano ya reli na barabara ya Nyerere eneo la Gold Star
jijini Dar es Salaam majira ya saa sita mchana leo gari hilo lilikuwa
likitokea maeneo ya Mnazi Mmoja lilielekea Tazara.
Askari huyo akisalimiana na abiria
aliyeshuka katika gari hilo badala ya dereva na baada ya hapo alimwachia
bila ya kumchukulia sheria yoyote kama wanavyofanya kwa madereva
wengine wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
ASKARI polisi anayedaiwa kuwa ni wa
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), alikumbwa na kigugumizi na kushindwa
kumchukulia sheria dereva wa gari dogo aina ya Corrona lenye namba T
297 AQE baada ya dereva wa gari hilo kukiuka sheria ya usalama
barabarani kwa kusimama kwenye reli katika makutano ya reli na Barabara
ya Nyerere eneo la Gold Star jijini Dar es Salaam majira ya saa sita
mchana leo gari hilo lilikuwa likitokea maeneo ya Mnazi Mmoja lilielekea
Tazara.
Awali askari huyo baada ya kubaini kosa
lililofanywa na dereva huyo alilipiga picha gari hilo likiwa katikati
ya reli wakati magari mengine yakiwa katika foleni.
Baada ya kupiga picha hiyo alimfuata
dereva wa gari hilo alimtaka dereva wa gari hilo aweke gari lake pembeni
ili aandikiwe faini.
Lakini kabla dereva huyo hajaweka gari
hilo pembeni abiria aliyekuwa amekaa siti ya mbele ya gari hilo
alitelemka na kujitambulisha kwa askari huyo ambapo walianza kusalimiana
na kumruhusu aondoke bila kuchukuliwa hatua yoyote kama wanavyofanya
kwa madereva wengine.
Akizungumzia tukio hilo dereva wa
daladala linalofanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Mnazi mmoja
alisema sheria ni msumeno hivyo hata anapobainika ndugu jamaa, au rafiki
wa askari kafanya kosa anapaswa kuguswa na sheria zilizopo.
"Yule jamaa kama sio askari polisi basi
anaweza kuwa mwanajeshi au usalama wa taifa ndio maana yule jamaa
aligwaya kumchukulia hatua" alisema dereva huyo.
Dereva huyo alisema kama kosa hilo
lingefanywa na dereva ambaye hafahamiki na askari huyo ni lazima
angelipa faini kwani hiyo ni kawaida ya askari hao kumkomalia mtu hata
akiomba kusamehewa.


