CUF kugharamia matibabu ya Maalim Seif

Wanachama
wa Chama cha Wananchi (CUF) wamesema wapo tayari kugharamia matibabu
ya Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim Seif Sharif Hamad.
Tamko
hilo limetolewa siku chache baada ya kuibuka taarifa kuwa kiongozi
huyo amesusa gharama za matibabu zinazotolewa na Serikali ingawa ni haki
yake kwa mujibu wa sheria kama kiongozi mstaafu.
Akizungumza
kwa niaba ya wanachama wenzake kisiwani Unguja jana, mmoja wa wanachama
wa CUF, Ali Abdallah Issa, alisema wanashangazwa na baadhi ya watu
kumpiga na kumsema kiongozi huyo ambaye alidai ni kiungo muhimu katika
kuwaunganisha Wazanzibari.
“Maaalim
ana haki zote za kuhudumiwa na Serikali na si vinginevyo. Lakini kwa
manyanyaso na kusimangwa kila kukicha sisi wanachama wa CUF tupo tayari
kugharamia matibabu ya kiongozi wetu.
“Na
hili si jambo geni, Maalim alikamatwa na kuwekwa kuzuizini. Je,
alipotoka alikuwa akitibiwa na SMZ? Jibu ni hapana ni fedha zake
mwenyewe binafsi pamoja na wana CUF ambao walikuwa mstari wa mbele
kumhudumia kiongozi wetu nasi sasa tutafaya hivyo ikiwa SMZ imeshindwa,”
alisema Ali.
Alisema kitendo cha Maalim Seif kusafiri nje ya nchi kwa matibabu bila ya huduma za Serikali hakileti picha nzuri.
Kuna hatari visiwa vya Zanzibar vikaingia katika mgogoro na kujengeka chuki hasa kati ya CUF na CCM, alisema.
‘’Iwapo
Maalim Seif amekwenda kwenye matibabu kwa gharama zake binafsi basi
inasikitisha sana kuona ni jinsi gani Katiba inavyoanza kukiukwa na kwa
kweli si jambo jema na halifai,” alisema.
Naye
Is-hak Said Makame, alisema Zanzibar imepita katika wakati mgumu hasa
baada ya kutokea migogoro ya siasa iliyotokana na Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba mwaka jana na ule wa marudio uliofanyika Machi 20,
mwaka huu.
“Maalim
hawezi kusemwa na hata kuonekana ni kiongozi anayetibiwa kwa fadhila
kama alivyotaka Rais Magufuli alipokuja hapa Unguja kwenye mikutano
yake. Sasa tunasema sisi CUF tutamlinda kiongozi wetu kwa hali na mali,”alisema Makame.
Alipotafutwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Biman
kujua Maalim Seif amepata wapi fedha kwa ajili ya safari ya nje ya
nchi kutibiwa.
Alisema hajui ni wapi kiongozi huyo alipopata fedha za matibabu.
“Katibu
Mkuu amekwenda India kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake
lakini nasi hatujui ni wapi amepata fedha. Ila atakaporejea nchini
itatolewa taarifa kwa kina kuhusu suala hili,” alisema Biman.
Maalim Seif yuko India na anatarajiwa kujerea nchini siku chache zijazo.


