Breaking News

Huyu ndio mwandishi wa habari aliyekamatwa na kuteswa DRC

Mwandishi mmoja wa habari amekamatwa na kupigwa vibaya nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo siku ya Alhamisi kwa kuripoti mkutano wa mgombea urais wa upinzani Martin Fayulu.

Hayo yanajiri wakati tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo imetangaza kuharisha uchaguzi mkuu kwa kipindi cha wiki moja siku tatu kabla ya tarehe iliyopangwa ya Disemba 23 kutokana janga la moto kuunguza sehemu kubwa ya vifaa vya kupigia kura.
Kulingana na kundi la kutetea haki za vyombo vya habari la JED mwandishi huyo wa habari Rodrigue Ndakazieka, anayefanya kazi na kituo cha radio cha jimbo la Kwilu alichukuliwa na polisi wakati alipokuwa akiondoka ofisini siku ya jumatano.

Kwa mujibu wa DW Swahili, Mwandishi huyo alilazimishwa kuingia kwenye gari la maafisa hao na kisha kupelekwa katika nyumba ya naibu kiongozi wa chama tawala katika jimbo hilo ambapo alifungwa kwa kamba na kuteswa kwa saa kadhaa kabla ya kusafirishwa kwenda mjini Kinshasa.
Msemaji wa polisi mjini Kinshasa amekataa kutoa maelezo yoyote kuhusiana na kisa hicho.  
Jean Bosco Diona, mkuu wa kituo cha redio ambacho mwandishi aliyekamatwa anafanya kazi amesema kituo hicho na miundombinu ya kurushia matangazo imezingirwa na maafisa wa serikali.

Bosco ameongeza,  “Tumepangua sehemu kubwa ya ratiba yetu ya matangazo na waandishi wetu wa habari wamelazimika kwenda mafichoni kutokana tu na kurusha moja kwa moja mkutano wa Martin Fayulu”
Jana Alhamisi jioni mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo, Corneille Nangaa alitangaza kuharishwa kwa uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike jumapili ijayo, hatua ambayo imezua wasiwasi wa kutokea machafuko
Uchelewashaji huo ni tukio jingine la karibuni kabisa katika miaka miwili ya panga pangua ya uchaguzi mkuu nchini DRC iliyosababisha mzozo mkubwa wa kisiasa na makabiliano ya kumwaga damu.
Mgombea wa urais wa upinzani Martin Fayulu amesema hakuna sababu za kueleweka za kuhairishwa kwa uchaguzi huo na kuongeza kuwa rais Joseph Kabila na mwenyekIti wa tume ya uchaguzi (CENI) Corneille Nangaa watawajibika kwa uamuzi huo.
Chama tawala kimeelezea kusikitishwa kwake na hatua ya tume ya uchaguzi ya kuahirisha uchaguzi.
Kikaya Bin Karubi, mshauri wa kidiplomisa wa Rais Joseph Kabila amesema kwamba ni jambo la kusikitisha kwamba kampeni yao imesitishwa mapema, lakini akaongeza kwamba wanaheshimu uamuzi huo wa tume ya uchaguzi.
Hali iliendelea kuwa tulivu mjini Kinshasa baada ya tangazo hilo la kuahirisha uchaguzi, lakini baadhi ya maduka yalifunga milango yake kwa tahadhari, yakiogopa kutokea machafuko.
Kwa upande wao wananchi wameomba kuweko na uchaguzi wa kuaminika katika mazingira yenye uchaguzi, ingawa wamesikitishwa na hatua hiyo ya kuahirisha uchaguzi.
”Tulikuwa tayari kupiga kura Jumapili tarehe 23 Desemba. Kuahirishwa huku tunakuchukulia kama mapungufu upande wa serikali.” Amesema kijana mmoja aliyezungumza na DW mjini Kinshasa.
”Tulikuwa tunapendelea uchaguzi ufanyike kama ilivyopangwa, usiahirishwe na kupelekwa mbali, kwani yapo matatizo mengine mengi.” Amelalamika mwingine.

Hatua hiyo ya kuuahirisha uchaguzi imekuja baada ya tume kufanya mashauriano na wagombea wote 21 waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais.