Breaking News

NAIBU WAZIRI AFUNGA MACHIMBO YA MCHANGA MKURANGA MKOANI PWANI


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani mara baada ya kufanya ziara Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani baada ya kuyafungia machimbo ya mchanga.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina ameagiza kufungwa kwa machimbo ya mchanga yaliyopo katika kijiji cha Kolangwa Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani kwa kile kinachodaiwa kusababisha uharibifu wa mazingira na mali.

Mpina ametoa agizo hilo la kufungwa kwa machimbo hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira mkoani Pwani mapema hii leo, ambapo amebaini uharibifu huo umechangiwa na Taasisi za Serikali ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Idara ya Madini na Baraza la Taifa na Usimamizi wa Mazingira NEMC, kwa kile alichokisema kuwa uchimbaji huo umefanyika bila wananchi kushirikishwa na haukuzingatia miundombinu na sheria ya Mazingira pia makazi ya watu.

Kufuatia mapungufu hayo, Mpina ameagiza Taasisi hizo za Serikali kufuatilia uharibifu uliofanywa kwa muda wa wiki mbili na kukaa pamoja na mfanyabiashara huyo anayemiliki machimbo hayo kuona namna ya kuondoa kero hiyo inayowakumba wananchi pia uchafuzi wa mazingira unaofanywa na machimbo hayo, hivyo amesema kama kuna hasara yeyote ili mfanyabiashara huyo kulipa gharama hizo.
Awali Naibu Waziri Mpina alitembelea kiwanda cha Azam kilichopo Mkuranga mkoani Pwani na kuwapongeza kwa utunzaji wa Mazingira sambamba na hilo pia ameagiza kiwanda hicho kupima Maji taka yanayozalishwa kiwandani hapo.