Gari la polisi lenye namba PT.1852 Toyota Land Cruiser limeacha njia na kupinduka huku likisababisha majeraha kwa baadhi ya askari waliokuwa ndani ya gari hilo. Ajali hiyo imetokea jana Jumanne majira ya saa kumi na nusu alasiri katika barabara ya Kanzugu-Mugeta,kijiji cha Bukore,kata ya Kanzugu,tarafa ya Serengeti,wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.
Taarifa za kuaminika zimeeleza kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na askari namba E.7560 CPL Hamis wakiwa wanatokea wilaya ya Serengeti kikazi wakielekea wilayani Bunda ndipo gari likaacha njia na kupinduka na kusababisha majeruhi kwa baadhi ya askari.
Majeruhi wa ajali hiyo ni pamoja na E.4063 CPL Chacha mwenye umri wa miaka 47 ambaye amepata maumivu kifuani,mguu na mkono wa kulia,G.4165 PC Jacob mwenye umri wa miaka 33 ambaye amevunjika paja la mguu wa kulia.
Wengine waliojeruhiwa ni G.4414 PC Joseph,G.7285 PC Jumanne,H.393 PC Barnabas na G.8440 PC Exaud. Majeruhi wote hawa wamelazwa hospitali teule ya Bunda.