RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MZEE NDESAMBURO

“Kwa
masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la
Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo kilichotokea leo tarehe 31
Mei, 2017 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi Mkoani
Kilimanjaro, Namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake
uliozingatia siasa za kistaarabu”
Hii
ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli aliyoitoa katika salamu zake za rambirambi kwa familia ya
Marehemu Philemon Ndesamburo, Viongozi na wanachama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na ndugu, jamaa na marafiki
wote walioguswa na kifo hicho.
Mhe.
Rais Magufuli amesema alifanya kazi na Marehemu Philemon Ndesamburo
wakati wote wakiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na wakati wote walishirikiana, kutaniana na anamkumbuka kwa namna
ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslai kwa
wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.
Mhe.
Dkt. Magufuli ameitaka familia ya Marehemu Philemon Ndesamburo na wote
waliguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu
na amemuombea Marehemu apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Mei, 2017


