Breaking News

POLISI 5 WAUAWA KWA BOMU NCHINI KENYA


Maafisa watano wa polisi nchini Kenya wameuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa barabarani kaskazini mashariki mwa mji wa Liboi karibu na mpaka na Somalia.

Shambulio hilo lilitokea karibu na eneo lile lile ambapo maafisa wengine wanne waliuawa katika shambulio jingine la bomu siku ya Jumatano ambalo kundi la Alshabab limekiri kutekeleza.

Maafisa wengine watano waliuawa katika mashambulio tofauti ya mabomu siku ya Jumatatu katika kaunti Jirani ya Mandera.

Kundi la wapiganaji wa Al-Shabab limefanya mashambulio kadhaa nchini Kenya katika siku za hivi karibuni.

Kundi hilo lenye makao yake makuu Somali linataka Kenya kuondoa majeshi yake yanayohudumu chini ya vikosi vya AMISOM.

Mwandishi wa BBC Mohammud Ali mjini Nairobi ameripoti kwamba shambulio hilo la Mandera lililenga gari la gavana wa kaunti hiyo Ali Roba.

Bwana Roba alichapisha katika ujumbe wake wa Facebook siku ya Jumatatu kwamba alipoteza mlinzi wake katika shambulio hilo.

Ni shambulio la tatu ambalo lilimlenga Ali Roba katika kipindi cha siku tatu.