Breaking News

AUDIO:MSIKILIZE KAMANDA WA POLISI MWANZA AKIELEZEA MADHARA YA TETEMEKO LILILOTOKEA MKOANI HUMO


Tetemeko la ardhi lililotokea katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita na Kagera, limesababisha kifo cha askari WP Koplo Joyce Jackson wa Kituo cha Polisi Misungwi.

Mbali ya kifo hicho, pia limejeruhi watu watatu wakiwamo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igokelo na mahabusu mmoja.

 Tetemeko hilo lililotokea juzi Alhamisi saa 6:55 mchana na kudumu kwa muda wa dakika moja, limesababisha taharuki kubwa katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na kwa baadhi ya wananchi wa mikoa ya Mwanza na Kagera ambao walilazimika kukimbilia ofisi zao kwa hofu ya kuangukiwa na majengo.

Shuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kutaja jina  amesema walikuwa  wamepumzika nje ya Kituo cha Polisi Misungwi,  baada ya kutokea tetemeko la ardhi na Koplo Joyce alidondoka chini na kupoteza fahamu.

Alisema walimsaidia kumkimbiza hospitali, lakini wakati wanamfikisha alikuwa tayari amefariki dunia.

“Joyce alianza kazi jana, baada ya kumaliza likizo ya uzazi. Alijifungua kwa njia ya upasuaji na ameacha kichanga, alikuwa pia  anasumbuliwa na shinikizo la damu (presha),” alisema shuhuda huyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Dk. Marcelina Kiemi, alithibitisha kupokea mwili wa Koplo Joyce na majeruhi ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igokelo na mahabusu mmoja.

“Baada ya kutokea tetemeko la ardhi, nimepokea mwili wa askari polisi wa kike Joyce Jackson ambaye alikuwa tayari amefariki dunia,” alisema Kiemi.

Dk. Kiemi, alisema majeruhi watatu; Anna Habi (18) mwanafunzi wa kidato cha nne, Mathayo Ndalahwa (15) kidato cha kwanza kutoka Shule ya Sekondari ya Igokelo na mahabusu Mathias Simoni (22) mkazi wa Kijima, wamelazwa na wote hali zao zinaendelea vizuri.

 Mwalimu wa Shule ya Sekondari Igokelo, Adela Sakoma, alisema wakati tetemeko hilo linatokea walikuwa darasani, ndipo wanafunzi walianza kukimbizana kutoka nje kupitia mlangoni ili kunusuru maisha yao.

Alisema baadhi yao walijeruhiwa na kuwakimbizwa hospitalini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kifo cha Koplo Joyce.

Alisema kwa muda sasa, Koplo Joyce alikuwa akisumbuliwa na tatizo la presha.

“Huyu WP Koplo Joyce alikuwa na tatizo la presha, wakati tetemeko linatokea wakiwa wanatoka nje, alianguka ghafla. Wenzake walimsaidia na kumkimbiza hospitalini na walipomfikisha tayari alikuwa amepoteza uhai,” alisema Kamanda Msangi.
Bofya hapa chini kumsikiliza kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza akifafanua kuhusu taarifa hii.