Breaking News

ASKARI WA CHINA WAPONGEZWA NA UN KWA JUHUDI ZAO NCHINI SUDAN KUSINI



 Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS imewapongeza walinda amani wa China kwa juhudi zao katika kuwalinda raia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa UNMISS Bw David Shearer katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya walinda amani wa Umoja wa mataifa yanayofanyika kila mwaka ili kuwaheshimu na kuwakumbuka walinzi wa amani waliopoteza maisha yao kazini. Akizungumza kwenye maadhimisho hayo huko Juba Bw. Shearer amesema licha ya kufanya kazi kwenye hali ngumu, walinzi wa amani wa China na wenzao wa nchi nyingine wamejitolea kuwahudumia watu wa Sudan Kusini, na baadhi yao wamepoteza maisha kazini. Amesema mwaka jana askari wawili wa China walipoteza maisha na wengine watano walijeruhiwa baada ya gari lao kushambuiliwa kwa guruneti.

Kikosi cha China chenye askari 700 kinahudumia chini ya tume ya UNMISS yenye jumla ya askari 12,000, ambao wana kazi ya kulinda raia, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, kutoa ulinzi na kufanya doria.