Rais Magufuli amepokea ripoti ya mwaka 2015/2016 ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyowasilishwa kwake jana na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola.
Katika maelezo yake mafupi kwa Mhe. Rais Magufuli, Kamishna Mlowola katika kipindi cha tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani fedha za umma zilizookolewa na TAKUKURU zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 7 hadi kufikia Shilingi Bilioni 53 huku kukiwa na mafanikio makubwa katika kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.
Amesema kutokana na nia thabiti ya Serikali ya Awamu ya Tano kukabiliana na rushwa wananchi wameitikia kwa wingi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi za rushwa ambazo zinafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU kuhakikisha wote wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua zinazostahili na kwamba kama kuna mapungufu ya kisheria ishirikiane na vyombo husika kurekebisha sheria hizo.
“Rushwa tukiiacha iendelee tutakwama, kwa hiyo niwaombe Watanzania na vyombo vyote vinavyohusika vitoe ushirikiano mkubwa kwa TAKUKURU, lakini nitoe wito kwenu TAKUKURU, sijaona watu wakifungwa sana kwa makosa ya rushwa.
"Mtu anashikwa na ushahidi lakini akipelekwa mahakamani ushahidi haupelekwi au unafichwa kwa makusudi au anayeendesha kesi anaamua kutokuusema halafu aliyeshikwa na rushwa anaachiwa, wananchi wanawajua wanaojihusisha na rushwa, ifike mahali watu wanaokutwa na makosa ya rushwa wafungwe” alisisitiza Rais Magufuli.