Mbowe Amvaa Rais Magufuli......Ashangazwa Kutumbuliwa Kwa Nape Nnauye na Kuachwa kwa RC Paul Makonda.

Ikiwa
ni siku ya tatu ya Bunge la Bajeti, jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, limeanza kusikika ndani ya mhimili huo wa dola baada ya Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kuhoji ukimya wa Serikali
juu ya tuhuma za vyeti feki, kumiliki mali nyingi zisizoendana na kipato
chake yakiwamo magari ya kifahari ya aliowatuhumu kuwa wafanyabiashara
wa dawa za kulevya na matumizi mabaya ya madaraka.
Akizungumzia
suala la vyeti, alisema Serikali inaendesha uhakiki wa watumishi wa
umma ikiwamo vyeti vya taaluma jambo ambalo ni jema, lakini ni muhimu
kazi hiyo ikafanywa kwa weledi bila kuathiri masharti ya Ibara ya 13 (1)
ya Katiba ya nchi inayoonya ubaguzi wa aina yoyote kwa mtu yeyote bila
kujali cheo chake, kabila lake, dini yake, elimu yake na hata jinsia
yake.
“Wapo
Watanzania wengi waliochukuliwa hatua baada ya kukutwa na vyeti feki,
lakini cha ajabu Rais ameendelea kumkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, ambaye anashutumiwa kutumia cheti ambacho si chake na kushindwa
hata kuamuru uchunguzi wa jambo hilo ufanyike, ni kitendo cha
kufedhehesha sana kwani kinawagawa Watanzania.
“Ubaguzi
wa namna hiyo unalifanya kundi fulani kujisikia wanyonge na hawana haki
na kundi jingine kujisikia wao wana haki zaidi ya wengine. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutenda haki katika zoezi hili la
uhakiki kwani limeshaanza kuonyesha dalili za ubaguzi na upendeleo na
linaweza kusababisha matabaka ya watu katika taifa,” alisema Mbowe.
Kiongozi
huyo alisema kambi yake inaunga mkono vita ya dawa za kulevya, lakini
hivi karibuni vita hivyo vilichukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya.
“Kitendo
cha kuwataja watu hadharani bila ushahidi wowote, kilifanywa kibabe kwa
kuwakejeli, kuwadhihaki na kwa uonevu mkubwa kwakuwa hakukuwa na
ushahidi wowote na pia mahakama haikuhusishwa katika hatua za awali. Hii
ina maana kwamba mkuu huyo wa mkoa aliamua kuwa hakimu kwa kutumia cheo
chake kuchafua majina ya watu na haiba waliyoitengeneza kwa muda mrefu
na kwa gharama kubwa.
“Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa sana na kitendo cha Rais
kuendelea kumkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam katika matukio
tofauti tofauti, huku ushahidi wa wazi ukionyesha matumizi mabaya ya
madaraka na ukiukwaji wa haki za binadamu, umiliki wa mali ulio wa
shaka, ikiwamo magari ya anasa ya wafanyabiashara aliowatuhumu
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, vitisho kwa vyombo vya
habari, kuingilia uhuru wa habari nchini, matumizi mabaya ya rasilimali
za nchi ikiwa ni pamoja na kufanya tafrija ya kutimiza mwaka mmoja
kazini kwa kivuli cha kampeni ya kutokomeza dawa za kulevya.
“Ni
jambo la kusikitisha sana kuona Rais akimtoa kafara waziri wake kwa
gharama ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Tunajiuliza kuna jambo gani
lililojificha baina ya Rais na Mkuu huyu wa Mkoa? Tatizo la madawa ya
kulevya si tatizo la mtu mmoja na wala halihitaji kufanywa kama vita ya
mtu binafsi.
“Kambi
Rasmi ya Upinzani inatambua Rais ana mamlaka ya kuteua na kutengua
uteuzi, lakini hana mamlaka ya kumkingia kifua mtu yeyote pale
anapovunja sheria za nchi, hata kama Rais ndie aliyempa dhamana. Hivyo
basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka viongozi wote waliopewa dhamana
kuheshimu utu na haki za kila raia.
“Ugomvi
binafsi, kutofautiana kiitikadi, kiimani na hata kimtazamo kusimfanye
yeyote mwenye dhamana kutumia mamlaka yake katika kumwonea mtu yeyote.
Kama taifa tuna jukumu la kusimamia misingi ya utu na kuheshimiana.
“Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mheshimiwa Rais kumchukulia hatua za
kinidhamu Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam. Aidha, Rais aache ubaguzi katika
uamuzi wa kinidhamu kwa baadhi ya viongozi wa umma, kwani hii ni kuwa na
‘double standard’ katika utekelezaji wa majukumu yake,” alisema mbowe.


