Haya Ndio Maajabu ya Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka Huu.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2017 zimezinduliwa rasmi leo katika
uwanja wa Kumbukumbu Mjini Mpanda mkoani Katavi na unatarajiwa kuzunguka
katika mikoa yote 31, ukipita kwenye halmashauri 195 kwa muda wa siku
195.
Katika sherehe hizo za uzinduzi, kiongozi wa mbio hizo kwa mwaka huu pia
ametangazwa rasmi, ambapo atakuwa ni Amour Amad Amour kutoka mkoa wa
Kaskazini Unguja visiwani Zanzibar.
Kiongozi huyo atasaidiana na wenzake watano katika kukimbiza mwenge huo
ambao ni pamoja na Bahati Mwaniguta Lugodisha (Geita), Bi Fatima Yunus
Hassan (Kusini Pemba), Fredrick Joseph (Singida), Salome Obadia
Mwakitalima (Katavi) na Shukran Islam Msumi (Mjini Magharibi).
Kauli mbiu ya mbio hizo kwa mwaka huu inasema "SHIRIKI KUKUZA UCHUMI WA VIWANDA KWA MAENDELEO YA NCHI YETU'
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni makamu wa pili wa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ali Idd kwa niaba ya Rais wa
serikali hiyo Dkt. Ali Mohamed Shein, ambapo katika ujumbe wake
amesisitiza umuhimu wa watanzania wote kuweka nguvu zao katika kujenga
taifa la viwanda
Amesema hadi sasa tangu serikali yake iingie madarakani kwa muhula wa
pili tayari viwanda vitatu vya watu binafsi vimekwishajengwa visiwani
Zanzibar
Balozi Seif amesema mbali na kaulimbiu ya mwaka huu kusisitiza umuhimu
wa viwanda, pia mbio hizo zitakuwa zikieneza ujumbe kuhusu mapambano
dhidi ya Malira, UKIMWI, Dawa za Kulevya pamoja na rushwa.
Mbio hizo zimeanzia katika wilaya ya Mpanda, na kilele chake kitakuwa ni Oktoba 14 katika mkoa wa Mjini Magharibi.
Kumbukumbu zinaonesha tukio kama hili la uzinduzi tangu mwaka 2011 lilikuwa kama ifuatavyo
2011 Butiama (Mgeni rasmi akiwa Mohamed Ghalib Bilal)
2012 Mbeya (Mgeni rasmi akiwa Mizengo Pinda)
2013 Pemba (Mgeni rasmi akiwa Dkt Ali Mohamed Shein)
2014 Kagera (Mgani rasmi akiwa Mohamed Ghalib Bilal)
2015 Ruvuma (Mgeni rasmi akiwa Dkt Ali Mohamed Shein)
2016 Morogoro (Mgeni rasmi akiwa Samia Suluhu Hassan)


