Dk. Slaa Azungumza Kwa njia ya Simu kuhusu Madai ya Kujiunga CUF
Wakati
mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ukizidi kutokota, Mwenyekiti
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu
Lipumba anadaiwa kutaka kumvuta aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Wilbroad Slaa, kujiunga na CUF.
Madai
hayo yameibuka baada ya kuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati ya Prof.
Lipumba na Dk. Slaa ambao kwa nyakati tofauti mwaka 2015, walijiondoa
kwenye vyama vyao kipindi cha mchakato wa kusaka mgombea urais wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa).
Ingawa
Dk. Slaa kaika mahojiano alikanusha habari za yeye kutaka kujiunga na
CUF, lakini habari zinasema kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba
amekuwa akihaha kumshawishi Dk. Slaa pindi atakaporejea nchini ajiunge
na CUF na kushika moja ya nafasi za juu za uongozi.
Taarifa
za kuaminika zilieleza kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba na DK.
Slaa yanalenga kuboresha safu ya uongozi wa chama hicho kwa kumpa
wadhifa wa Ukatibu Mkuu au Umakamu Mwenyekiti licha ya kudaiwa kwenda
kinyume cha Katiba iliyoanzisha CUF.
Kwa
mujibu wa katiba hiyo, nafasi za juu za uongozi wa chama hicho
zinatakiwa kuzingatia uwiano wa pande mbili za Muungano. Endapo
mwenyekiti anatoka Bara, Katibu Mkuu atatoka upande wa pili wa Muungano.
Baadhi
ya wana CUF wanaomuunga mkono Prof Lipumba wamekiri kuwa kumekuwa na
mawasiliano ya wawili hao, huku wakisema hakuna anayejua kiini cha
kuimarika kwa mawasiliano hayo wakati huu ambapo CUF imepasuka katika
makundi mawili, moja likiongozwa na Katibu Mkuu Maalim Seif na jingine
lipo chini ya Lipumba.
Msemaji
wa CUF inayoongozwa na Maalim Seif, Mbarala Maharagande, amesema kuwa
taarifa za kurudi kwa Dk. Slaa amezisikia japo hajui atajiunga na chama
gani.
“Labda
wale watu wa Lipumba ukiwauliza wanaweza kukuhakikishia hilo. Kwa
nafasi ya katibu itakuwa ngumu kwa sababu katiba yetu hairuhusu, lakini
kuwa mwanachama anaweza. Nguvu ya Lipumba ilishapungua sana na wenye
chama chao (wananchi) watakwenda kukichukua na kumtoa ofisini kwa hiyo
kama anarudi Dk. Slaa kuja kuongezea nguvu upande huo inawezekana”. alisema Maharagande.
Akizungumza
kwa njia ya simu, Dk Slaa aliyekuwa Mbunge wa Karatu alisema taarifa
hizo si sahihi kwani alishaahidi kwamba hatarudi kwenye siasa za vyama.
Alisema
hawezi kuyumba kwenye uamuzi wake licha ya kukataa kuweka wazi kwamba
ni lini atarejeea nchini, alisisitiza kuwa msimamo wake wa kuachana na
siasa za vyama uko palepale.
“Maneno
yangu hayayumbi, sitafanya siasa za vyama, nimeachana nazo. Naomba
msiniingize kwenye siasa uchwara, sizifanyi hizo… Saisa ni ajenda. Hizo
siasa za kishabiki zifanyeni nyinyi huko Tanzania, mimi sifanyi
ushabiki, hakuna mtu anayekula ushabiki, ndiyo maana siasa zangu siku
zote ni ajenda, Watu wanataka maji, wanataka chakula, wanataka elimu
bora, si ushabiki”
“Kwa miaka 20 niliyokuwa kwenye siasa sijawahi kufanya ushabiki, nilitafuta ajenda na kuipanga mikakati kwa ajili ya wananchi” alisema Dk Slaa alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema
atasimama kupiga kelele kwa ajili ya Tanzania pale atakapoona mambo
yanakwenda kombo na atafanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa si siasa.
Septemba
25, 2015 akizungumza na wandishi wa habari kwa zaidi ya saa 2 kisha
kutangaza kujitoa Chadema, alisema ni afadhali apotee kwenye ulimwengu
wa siasa duniani kuliko kumuunga mkono Lowassa.