Bosi wa Freemason Tanzania, Sir Andy Chande Afariki Dunia.

Aliyekuwa
Kiongozi wa Jumuiya ya Freemason Tanzania na Afrika Mashariki, Sir
Jayantilal Keshavji ‘Andy’ Chande, amefariki dunia.
Sir Chande amekuwa mwanachama wa Freemason kwa takribani miongo sita tangu ajiunge na umoja huo mwaka 1954.
Kiongozi huyo alizaliwa Mombasa, Kenya Mei 7, 1928 ingawa wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene Mjini mkoani Tabora.
Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana asubuhi.
Kulingana na taarifa hizo, kiongozi huyo alifariki dunia jijini Nairobi, Kenya alikokuwa akitibiwa.
Kiongozi huyo aliwahi kueleza kuwa alijiunga na Freemason Oktoba 25 mwaka 1954 baada ya kupitia usaili.
Aliwahi
pia kutunga kitabu alichokiita kwa jina la ‘A night in Africa –journey
from Bukene’ (usiku wa Afrika – safari kutoka Bukene).
Katika
miaka ya 1950 ndipo alieleza kuanza kutambua kuwa Freemason ipo katika
msingi wake, ikiwa ni pamoja na sayansi ya maisha ambayo malengo yake
ni kumbadilisha mtu kiimani na kumfanya awe anavyopaswa kuwa.
Aliwahi
kuelezea kanuni tatu kubwa za Freemason ikiwa ni pamoja na kumtaka mtu
kuwa mkweli na mwenye maadili ambayo hasa Freemason inalenga kuyaweka
kwenye akili ili mwanachama awe mzuri.
Ngazi
ya pili ya utaratibu inatilia mkazo kwenye vipaji na akili kupitia
sanaa na sayansi ili kutoa mchango mzuri iwezekanavyo katika maisha.
Ngazi
ya tatu alisema kuwa unafundishwa namna ya kufurahia maisha kwa kiwango
chake cha juu kwa kufuata kanuni hizo na mwisho ni upendo wa kindugu,
kujiweka huru na ukweli.
Katika masha yake aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Shaaban Robert.
Akiwa
kwenye Jumuiya ya Freemason katika uhai wake, Sir Chande aliwahi pia
kukutana na viongozi mashuhuri nchini kama vile Rais wa kwanza wa
Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, marais wastaafu, Ally Hassan Mwinyi,
Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na msanii maarufu wa muziki wa Bongo
Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Hata
hivyo kutokana na fikra zilizojengeka katika jamii, Freemason ilikuwa
ikiogopwa na kutajwa tajwa na watu vibaya, mojawapo ikiwa ni kupata
utajiri kwa njia isiyo ya kawaida.
Hata
hivyo, hadi sasa dhana hiyo inaendelea na hakuna lililo wazi katika
hili, huku katika mitandao ya kijamii kila mmoja akijadili jumuiya hiyo
kadiri anavyoifahamu au kuisikia.
Histora yake
Sir
Chande alizaliwa Mombasa, Kenya Mei 7, 1928, ingawa wazazi wake
walikuwa wakiishi Bukene mkoani Tabora, magharibi mwa Tanzania.
Alifika
Tanzania mwaka 1950, alihamia Dar es salaam 1953 na kukutana na watu
wengi wa bandarini, shirika la reli na mashirika mbalimbali aliyofanyia
kazi.
Katika
simulizi zake kadhaa, Sir Chande alisema alikutana na watu wengi ambao
walikuwa wanahudhuria vikao vya Freemason, akaanza kuulizia na
akajifunza mambo kadhaa kuhusu watu hao.
Wakati huo, hao watu hawakuwa huru kuzungumzia Freemason kama alivyofanya Sir Chande, hasa kabla ya vita ya pili ya dunia.
Sir
Chande alisema wakati huo Freemason ilikuwa imegawanywa makundi
tofauti, katika hospitali, shule, na mashirika mbalimbali na kulikuwa na
kundi maalumu kwa ajili ya matajiri na wafanyakazi wakubwa wa Serikali.
Ukiangalia vizuri wengi wao walikuwa ni wazungu na baadhi ya Wahindi.
Kundi
la kwanza lilikuwa linaongozwa na watu wa Scotland, makundi mawili
yaliyofuata yalikuwa yanaongozwa na Waingereza na kundi la nne lilikuwa
linaongozwa na Wahindi ambalo ndilo Chande alilojiunga nalo. Ilimchukua
miaka miwili kukubaliwa kujiunga na Freemason.
Aliapishwa
rasmi mwaka 1954 akiwa na umri wa miaka 28. Kumbuka kwamba masharti ya
kujiunga ni lazima uwe na umri kuanzia miaka 21.
Baada
ya hapo ndipo alipanda cheo na kupewa nafasi ya kuongoza kundi au tawi
la Freemason katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania,
Uganda, Rwanda na Burundi.
Akajiunga
na miradi tofauti ya Freemason nchini Uingereza yakiwemo hoteli za
kifahari pamoja na kupewa jukumu la kujenga hoteli mpya ya Freemason
nchini Ghana kwenye Mji wa Khumasi ambayo ni ya kifahari.
Hoteli nyingine ya kifahari aliyoisimamia ujenzi wake iko Zambia.
Sir
Chande anakumbukwa sana kwa kuanzisha shule ya msingi ya Viziwi
Buguruni, Dar es Salaam, moja ya taasisi ambazo alizipa kipaumbele mno
hadi anaingia kaburini.
Sir
Andy Chande alistaafu kama kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki mwaka
2005 baada ya kuifanyia kazi kwa miaka 19, akawa hahudhurii mikutano ya
nchi hizi, lakini akishiriki ile ya Uingereza kwa sababu alikuwa
akiendelea kufanya kazi na mashirika ya huko.
Freemason ni nini?
Freemason ni taasisi kongwe, kubwa na inayotambulika kote duniani.
Pamoja
na kwamba shirika hili katika muundo wake wa sasa lilianzishwa mjini
London, Uingereza mwaka 1717, lakini historia yake inaelezwa kurudi
nyuma katika karne ya 14.
Limekuwa
likitajwa kwa kila aina ya minong’ono kiasi kuwa baadhi ya matapeli
wamekuwa wakiitumia fursa hiyo kujinufaisha, ikiwamo kutoa matangazo ya
kualika watu kujiunga wakilenga kukusanya fedha za ada kwa minajili ya
kuwafanya wanachama hao tarajiwa kuwa tajiri, wenye nguvu na ushawishi.
Licha
ya marehemu Chande na viongozi wengine duniani kuizungumzia kwa uzuri,
lakini bado Freemason inabakia fumbo tata miongoni mwa watu wengi
duniani wakiwamo Watanzania.
Kwa
mujibu ya vitabu vya historia, Freemason kama neno linavyojieleza kwa
Kiingereza, awali lilikuwa kundi la mafundi waashi (masons) au wajenzi
kwa maneno mengine.
Walikuwa wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa mahekalu na mabenki katika zama za kati.
Mejengo
mengi ya kale kama vile makanisa, mji wa Rome, Washington DC
ilisanifiwa na kujengwa na mafundi hawa ndiyo maana mengi yna alama zao.
Lakini
pia vitabu vya historia vinaeleza waashi hawa kutokana na uaminifu wao,
walikabidhiwa masuala ya utunzaji fedha za asasi mbalimbali kubwa hasa
benki na Kanisa Katoliki.
Wakati wakijenga mahekalu, pia walitengeneza mahandaki ya kuhifadhi fedha na kuzikia.
Utaalamu
wao wa ujenzi ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ukiingia ndani ya hayo
mahandaki bila ramani unaweza kupotelea humo ndani usiweze kutoka tena.
Kwa sababu ya kuwa waashi, alama zao kubwa ni vifaa vya ujenzi kama vile pima maji.
Ikatokea
kipindi ambapo hawa Freemason wanadaiwa kuasi na kuanza kujishirikisha
na mambo ya nguvu za giza, utoaji kafara watu na ushirika na shetani.
Wengine wanasema walianza kuiba fedha za Kanisa Katoliki, lakini ukweli halisi haujulikani.
Kutokana na sababu hizi na nyingine ambazo ni siri kati ya Kanisa na Freemason, wakafukuzwa kutoka ukatoliki.
Ndiyo sababu ambayo inaelezwa kutokuwapo kwa maelewano kati yao na Wakatoliki pamoja na imani nyingine duniani.
Wakatoliki walianzisha shirika jingine badala ya Freemason lijulikanalo kama Jesuits.
Hata hivyo, Freemason ya sasa inaelezwa tofauti na viongozi wake wengi duniani, akiwamo marehemu Sir Chande.
Inajieleza
kama taasisi ya kirafiki na kifamilia inayounganisha wanaume wenye
tabia nzuri wa dini tofauti, wenye kuchangia imani moja katika ubaba wa
Mungu na undugu duniani.
Utamaduni
wa Freemason unaanzia wakati wa ujenzi wa hekalu la Mfalme Solomon na
sherehe zake za kirafiki hutumia kazi za uashi kuashiria somo la maadili
na ukweli.
Uanachama
wa Freemason hauingiliani na imani ya mtu, familia au ajira yake na
hivyo ni kundi lisilo la kidini wala kisiasa ambalo linakaribisha watu
wa imani zote kwa malengo ya kuleta ustawi katika jamii.
Katika
miaka ya 1990, Freemason ilipata changamoto kubwa nchini Kenya baada ya
Rais, Daniel arap Moi kuunda tume kuchunguza watu wanaoabudu shetani,
ambayo moja ya majukumu ya tume yalikuwa kuichunguza Freemason.
“Nilifika
mbele ya tume hiyo mara mbili na katika nyakati tofauti kama Mkuu wa
Freemason Afrika Mashariki. Nilitoa ushahidi kuhusu kazi tunazozifanya,” alikaririwa Sir Chande akisema wakati huo.
Ijapokuwa
tume hiyo haikutoa majibu ya kazi waliyokabidhiwa na Rais Moi,
inasemekana ilisafisha tuhuma zilizoelekezwa kwa Freemason.
“Nafurahi
kusema kwamba tuhuma zile zilisafishwa zaidi na Rais aliyefuata
baadaye, Mwai Kibaki ambaye katika moja ya hotuba zake, alisema
Freemason imetoa mchango mkubwa sana nchini Kenya,” Sir Chande aliwahi kukaririwa akisema.


